Wednesday, 3 August 2016

RAIS MAGUFULI AWAKA

RAIS Dk. John Magufuli amewaonya walimu wa shule za msingi na sekondari wanaoghushi majina ya wanafunzi ili wapate fursa ya kutafuna fedha za mpango wa elimu bure zinazotolewa na serikali.

Ameagiza wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na maofisa elimu nchini, kusimamia fedha hizo na kuhakikisha idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika shule zote ni sahihi na kuwashughulikia walimu walioandikisha majina hewa, vinginevyo atawatumbua wao.

Pia, amewataka wabunge ‘wanaolilia’ baadhi ya miji sasa, ukiwemo wa Katoro, ipewe hadhi ya wilaya au halmashauri, waondokane na mawazo hayo kwani anataka serikali ibane matumizi ili wananchi wapate huduma bora na maendeleo.

Rais Dk Magufuli alitoa maagizo hayo kwa nayakati tofauti jana, wakati akihutubia wananchi kwenye uwanja wa Mnadani, katika mji mdogo wa Katoro, ulioko wilayani Geita na Katani Bwanga, wilayani Chato.

“Natoa onyo, baadhi ya walimu wameanza kuandika wanafunzi hewa. Wanaofanya hivyo wanatafuta matatizo, msijaribu kula fedha za serikali,” alisema Dk Magufuli na kuagiza fedha hizo zijulikane zinaenda kwa nani, maana hataki mwanafunzi yeyote apunjwe haki yake.

Alisema itafika mahali atakuwa anafanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye shule yoyote na iwapo atabaini kuna wanafunzi hewa, aliyefoji atakiona cha moto na wakuu wa wilaya watakaoshindwa kufuatilia na kujua idadi ya shule na wanafunzi wake, watakuwa hawatoshi.

“Wakurugenzi na ma DC, RC na ma DEO, lazima mkae macho katika fedha hizo ili zikiliwa, walaji nao waliwe, maana serikali inatoa shilingi
bilioni 18.77, kila mwezi kwa ajili ya mpango huo wa elimu kila mwezi kwa ajili ya kulipia karo, kununua chaki na matumizi mengineyo,” alisema Rais Magufuli alipokuwa katika mji wa Katoro.

Rais Magufuli aliahidi kuendelea kutekeleza ahadi zote alizotoa kwa wananchi wa jimbo la Busanda na mji huo wa Katoro, isipokuwa kuupa hadhi ya wilaya kama ambavyo baadhi ya mabango aliyoonyeshwa na wananchi yalivyokuwa yakiomba.

“Hakuna sababu ya kuwa wilaya wakati wananchi wanataka huduma. Hizo fedha za kununulia gari la DC na mkurugenzi afadhali zinunue dawa na kujenga zahanati au kuboresha huduma mnazohitaji,” alisema na kuwahoji wananchi wanataka huduma au DC, wakamjibu huduma.

Alifafanua kwamba, wakati akiwa waziri, alikuwa akidhani kutengeneza wilaya au halmashauri ni njambo rahisi, kumbe wakati mwingine ni kuongeza mzigo wa kuhudumia wananchi kwani anataka abane matumizi wananchi wapate maendeleo.

“Nawaomba wabunge wengine katika maeneo mengine, wasiniombe wilaya, waombe huduma. Natamani hata mikoa ingepunguzwa ili fedha zinazotumika kuiendesha zitumike kuboresha huduma za wananchi,” alieleza Rais Magufuli na kuongeza kuwa, hata wana Chato waondokane na ndoto za kutaka wilaya hiyo iwe mkoa, waote maendeleo kwanza.

Akizungumza na wananchi wa Bwanga, Rais Magufuli alisema ufaulu wa watoto katika shule haujawa mzuri, hivyo kuwaomba wazazi wawe wakali kwa watoto wanaochezea masomo na kufanya utoro huku akiwasisitiza wanafunzi watumie fursa hiyo kusoma kwa juhudi.

“Wazazi watunzeni watoto vizuri, muwe wakali na kuhakikisha wanaenda shuleni kupata elimu. Fedha zinaniuma, zikipotea bure wakati watoto wanaenda kwenye madisco,” alieleza na kusisitiza kuwa, watoto wasiposoma ipasavyo, taifa halitapata wataalamu wa kutosha.

Rais Magufuli alisema serikali itaendelea na juhudi za kuboresha huduma za jamii, ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya cha kaya hiyo ya Bwanga, kutokana na fedha za bajeti ya afya ya mwaka huu na kuwataka wananchi watimize wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii. Alisema wajibu wa serikali ni kuwajengea uwezo na kuwawezesha kiuchumi. 

Awali, mbunge wa Busanda, Lolesia Bukwimba, akitoa salamu kwa wananchi wa Katoro na Buselesele, alimuomba Rais Magufuli akumbuke ahadi alizotoa wakati wa kampeni na kusaidia kuharakisha umeme katika maeneo, ambayo hayajapata huduma hiyo, likiwemo eneo la Mnadani.

Pia, aliomba mji wa Katoro upewe hadhi ya wilaya, kupatiwa maji ya Ziwa Victoria, kuboresha huduma za kituo chake cha afya na kujenga barabara, ikiwemo ya Katoro - Ushirombo kwa kiwango cha lami.




No comments:

Post a Comment