Thursday, 19 January 2017

SILAHA ZA KIVITA, NYARA ZA SERIKALI ZAKAMATWA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameshuhudia silaha 61 za aina mbalimbali, zikiwemo za kivita na nyara za serikali zenye thamani ya zaidi ya sh. miilioni 120, zilizokamatwa hivi karibuni mkoani Tabora.

Baada ya kushuhudia lundo la silaha hizo na nyara mbalimbali, Waziri Mwigulu alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi na maofisa wa maliasili mkoani humo.

Aliwataka maliasili na askari polisi kuendeleza mshikamano ili kukomesha vitendo vya ujangili na ujambazi, ikiwemo kuhakikisha silaha zote zilizogaa mitaani zinakamatwa.

"Maliasili mna dhamana kubwa ya kulinda usalama wa rasilimali zilizoko katika hifadhi za serikali, vivyo hivyo kwa polisi, endeleeni na msako huo ili kuhakikisha silaha zote zinazozagaa, zinakamatwa mara moja," alisema Mwigulu.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, ACP Hamis Seleman, alimweleza waziri kuwa silaha hizo zilikamatwa kutokana na operesheni maalumu iliyofanywa kwa kushirikiana na maofisa wa maliasili mkoani Tabora.

Alisema silaha zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni SMG 12, Rifle 6, Shortgun 2, Magobole 41, risasi za SMG 47 na maganda yake matatu, maganda ya Rifle matano na vichwa vya risasi za Rifle vitatu, ikiwemo nyara za serikali zenye thamani ya sh. 120,595,800 na mbao za sh. 10,972,581.

Alitaja silaha nyingine zilizokamatwa na askari polisi na kusalimishwa katika operesheni maalumu, iliyofanywa na askari wake katika wilaya saba za mkoa huo, kuwa ni SMG 6, Rifle 4, Shortgun 11 na Gobole 136.

Alibainisha kuwa katika msako huo, watuhumiwa 35, walikamatwa na kesi 21, zimefikishwa mahakamani katika kipindi cha kuanzia Septemba 22, mwaka jana, hadi sasa.

Alisema operesheni hiyo ililenga kupambana na majangili na wafanyabiashara haramu wa nyara  za serikali na iliongozwa kwa taarifa za kiintelejensia zilizofanywa kistaarabu pasipo kutumia nguvu kubwa.

RPC alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo wanaomiliki silaha kinyume na taratibu, kuzisalimisha kituo cha polisi kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kuomba wananchi watoe taarifa za watu wanaomiliki silaha hizo.

Kaimu Mkurugenzi wa Wizara wa Maliasili na Utalii, Profesa Alexander Songorwa, alisema kukamatwa kwa silaha hizo na nyara za serikali ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na taasisi zake za TAWA, TANAPA, NCAA na TFS kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Alisema wizara imeanzisha mfumo maalumu wa kupambana na ujangili na uvunaji haramu wa mazao ya misitu, ambapo nchi imegawanywa katika kanda tisa za doria za kiikolojia, ambazo ni Selous Kaskazini na Selous Kusini, Serengeti, Burigi-Biharamulo-Rubondo na Katavi-Rukwa-Mahale.

Profesa Songorwa alizitaja kanda nyingine kuwa ni Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha (Momela), Tarangire-Manyara, Ruaha-Rungwa na Moyowosi-Ugalla, inayojumuisha wilaya zote zinazozunguka mapori ya akiba ya Moyowosi, Kigosi na Ugalla.

Alitaja wilaya hizo kuwa ni Kibondo, Kakonko, Kaliua, Urambo, Sikonge, Uyui, Tabora, Mlele, Nsimbo, Mbogwe, Ushetu na Bukombe.

No comments:

Post a Comment