Thursday 19 January 2017

JAJI MKUU MPYA AAPISHWA, ATAJA MIKAKATI YAKE


RAIS Dk. John Magufuli, amemwapisha Jaji Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambapo baada ya kuapishwa, kiongozi huyo alieleza mambo atakayotilia mkazo katika kuendeleza maboresho kwenye sekta ya mahakama nchini.

Miongoni mwa mambo hayo ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kusimamia mpango mkakati wa maendeleo ya mahakama, usajili wa kesi kwa kutumia mfumo wa kieletroniki, uendeshwaji na utolewaji maamuzi ya kesi kwa uwazi.

Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam, jana, Jaji Profesa Juma, ambaye ni mbobezi kwenye sheria za kijamii, alisema mahakama inapaswa kuendelea kuwahudumia wananchi kwa kutoa haki haraka na uwazi zaidi.

“Majaji waliopita, waliweka misingi ya mabadiliko kwenye mahakama, hivyo misingi hiyo lazima iendelezwe kwa kufuata mpango mkakati wa mahakama.

“Nilipata bahati ya kusoma Sera ya Taifa ya TEHAMA, ambayo inaeleza wazi kama taifa katika kipindi cha miaka 20 ijayo, tunapaswa kuwa wapi. Nitatilia mkazo matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha kazi mbalimbali, zikiwemo usajili wa kesi kieletroniki, utakaosaidia uendeshwaji wake,” alieleza.

Kwa upande wake, Jaji mstaafu Othman Chande alisema motisha kwa wafanyakazi wa mahakama ili kuwafanya watumishi wa nguzo hiyo muhimu kufahamu jukumu lao la kuwatumikia wananchi, ni baadhi ya mambo yaliyompa changamoto wakati akiwa kwenye wadhifa huo.

Alisema alifanikiwa kuifanya mahakama kufanya kazi kwa malengo kama ilivyoainishwa kwenye mpango mkakati wa mahakama.

“Kwa mipango tuliyokuwa tumeiweka, hata kasi iliyokujanayo serikali ya awamu ya tano, haikuistukiza mahakama kwa sababu ilikwishaanza kwenda kwa kasi,” alisema.

Aliyataja baadhi ya mambo yaliyopo kwenye mpango wa maendeleo wa mahakama, ambayo yalisaidia kuongeza kasi ya uendeshwaji kesi kuwa ni maboresho ya miundombinu ya mahakama, ushirikishwaji wa polisi, ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ofisi ya Mwendesha Mashitaka na Jeshi la Magereza.

“Pia mahakama imeweka mfumo wa kupokea malalamiko nchi nzima ili kuwatendea haki wananchi kwa uwazi,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu Mahakama ya Mafisadi, alisema mahakama hiyo imeanza kupokea maombi matatu ya dhamana na mwaka huu, huenda ikaanza kusikiliza kesi za namna hiyo.

Jaji mstaafu Chande alisema mahakama hiyo licha ya kuwa kwenye ngazi ya mahakama kuu, lakini ina taratibu zake, ambapo kesi ili ifikishwe kwenye mahakama hiyo, lazima upelelezi wake uwe umekamilika.

Jaji mstaafu Chande alieleza taratibu zingine kuwa ni usikilizwaji wake unapaswa kuchukua mwezi mmoja ili uamuzi utolewe kwa haraka.

“Kesi za ufisadi zina ugumu wake kwa sababu, zinahitaji ushahidi wa kutosha, wakati mwingine itahitaji taarifa za kibenki, idadi kubwa ya mashahidi pamoja na kuhusisha makosa mengi ya jinai,” alifafanua.

Alieleza kuwa bado kesi za ufisadi zinaweza kufunguliwa kisha kusikilizwa kwenye kanda zote 13 za mahakama kuu.

Rais Dk. Magufuli amemteua Jaji Profesa Juma kushika wadhifa huo, baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Othaman Chande, kustaafu. Kabla ya kushika wadhifa huo, Profesa Juma alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Pia, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Sheria, mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Kitivo cha Sheria.

No comments:

Post a Comment