Thursday 19 January 2017

MAJALIWA AIBEBESHA ZIGO WIZARA YA ELIMU


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi  wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwenda Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizofanya shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
                                                                            
Pia, ameziagiza halmashauri nchini, kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha inawasimamia vizuri walimu, jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi, alipowasili Ikulu Ndogo ya Mpanda, kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka Mtwara na moja Tanga.

Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka  huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.

“Viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI, waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10, zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana, zitoke huko,”alisisitiza.

Mbali na kuuagiza uongozi wa wizara hizo kwenda Mtwara, pia Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wasimamie vizuri mikoa, ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki, badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.

Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga, alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana, mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na Geita.

Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu, wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.

No comments:

Post a Comment