Tuesday 15 November 2016

MAHAKAMA YAMWACHIA HURU NDASSA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, aliyekuwa akituhumiwa kuomba rushwa ya sh. milioni 30, kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Felchesmi Mramba.

Ndassa, aliachiwa huru jana, mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya kutajwa.

Ndassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji, alipandishwa kizimbani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akituhumiwa kuomba rushwa hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa huyo alikuwa akidaiwa kutenda makosa hayo, Machi 13, mwaka huu, Dar es Salaam.

Shitaka la kwanza, Ndassa alikuwa akidaiwa kwamba, akiwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji, aliomba rushwa ya sh. milioni 30, kutoka kwa bosi huyo wa TANESCO.

Ilidaiwa aliomba rushwa hiyo kama kishawishi ili aweze kuishawishi kamati yake iweze kutoa hati safi  ya ukaguzi wa ripoti ya Hesabu za mwaka 2015/2016, kwa shirika hilo.

Pia,  ilidaiwa alimshawishi Mramba kumpatia umeme ndugu yake Ndassa, alitambulika kwa jina la Matanga Mbushi na rafiki yake Lameck Mahewa, akimshinikiza atoe huduma hiyo ili kamati yake iweze kutoa hati safi ya ukaguzi wa ripoti ya hesabu ya mwaka 2015/2016  kwa shirika hilo.

No comments:

Post a Comment