Tuesday 15 November 2016

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WATOTO KUTEMBEA USIKU PEMBA


MKUU wa Wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid, amepiga marufuku watoto waliochini ya umri wa miaka 18, kutembea zaidi ya saa mbili usiku, katika shehia za Mjini Wete, ili kudhibiti vitendo vya udhalilishaji na kujenga maadili mema kwa watoto.

Amesema serikali ya wilaya yake imelazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ulawiti, wizi na utumiaji wa dawa za kulevya, vinavyofanywa na watoto wadogo mitaani na katika maeneo ya skuli.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, wakati akizungumza na wananchi wa shehia ya Kizimbani, Mtemani, Jadida na Bopwe, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kutekeleza mikakati ya kupambana na vitendo viovu.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya aliwasisitiza wananchi kujenga ushirikiano na serikali ili kuwabaini watoto wenye tabia hiyo ili wachukuliwe hatua, ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika malezi ya watoto.

“Kuanzia leo, ni marufuku kwa watoto waliochini ya umri wa miaka 18, kutembea usiku zaidi ya saa mbili. Hii ni katika mikakati ya kudhibiti vitendo vya uhalifu pamoja na ulawiti,”alisema.

Mkuu huyo wa wilaya  aliwataka wananchi wa shehia hizo, kuunda kamati za maadili na kanuni zake, ambazo zitatumika kuwabana wahusika wa vitendo hivyo, ambavyo vinaendelea kuathiri vijana, ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Rashid alisema serikali imesikitishwa na kukithiri kwa matendo hayo, hususan ulawiti na kuongeza kwamba, wamejidhatiti kuhakikisha wanayatokomeza makundi na kuusambaratisha mtandao wa vijana wanaojihusisha na  vitendo hivyo.

Kwa upande wao, wakazi wa shehia hizo walisema kuwepo kwa vitendo vya ushoga na matumizi ya dawa za kulevya na pombe, ni chanzo cha kuporomoka kwa maadili kwa watoto wao.

Khamis Faki, akizungumza kwa niaba ya wenzake katika kikao hicho, aliiomba serikali kuwa na dhamira ya kweli juu ya mikakati na malengo yake ya kupambana na vitendo hivyo, na kuongeza kwamba, wako tayari kushirikiana nayo pamoja na vyombo vya sheria kufanikisha azma hiyo.

“Kwa hili, serikali tunaiunga mkono kwa asilimia zote, lakini tunaitaka iwe na dhamira ya kweli kwani vitendo vinavyofanywa na vijana vina athari kubwa na sisi wazazi tuko pamoja na serikali," alisema.

No comments:

Post a Comment