Tuesday 15 November 2016

WAHAMIAJI HARAMU WASAKWE KILA KONA-MWIGULU NCHEMBA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amefanya ziara kwenye ofisi za makao makuu ya Idara ya Uhamiaji na kuagiza wahamiaji wanaokiuka sheria za kuwepo nchini, wasakwe kila kona, kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema kitendo cha mtu, ambaye si Mtanzania kuwepo nchini na kukiuka sheria na taratibu anazopaswa kuzifuata ili kuendelea kuwepo, hakuna mjadala na kwamba, Idara ya Uhamiaji iweke mkazo kwenye oparesheni zake nchi nzima.

Pia, ameagiza uongozi na watumishi wa idara hiyo nyeti, kutokumuonea mtu kwenye utekelezaji wa majukumu yao, badala yake watangulize uadilifu ili kuepuka lawama na kuchafua taswira ya ofisi hiyo.

Pamoja na hayo, amewataka watumishi 10 wa kitengo cha utumishi kwenye idara hiyo, kufika ofisini kwake leo, saa mbili asubuhi, baada ya kubaini uwepo wa uzembe uliosababisha baadhi ya watumishi kutopata haki zao za maslahi ipasavyo.

Akizungumza na baadhi ya watumishi kwenye ukumbi wa mikutano wa idara hiyo, Kurasini, jijini Dar es Salaam, jana, ambako alizuru kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo, alisema Idara ya Uhamiaji ni muhimu na inapaswa kuheshimiwa.

Mwigulu alisema tangu amekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ametembelea taasisi zote zilizoko chini yake ngazi ya mikoa na kwamba, kwa sasa amegeukia makao makuu, ambako anazungumza na watumishi na wateja kujua kero zao.

Alisema jana, alipofika kwenye ofisi hizo, alikuta misururu ya watu wanaosubiri huduma  ya uhakiki wa malipo, ambayo tayari yamefanywa kwenye benki mbalimbali, jambo ambalo wateja nao walililalamikia kuwa linapoteza muda.

"Nilipofika hapa kwenu, hapo ghorofa ya chini nilikutana na msururu wa watu wanaosubiri kufika dirishani kuhakikiwa malipo yao, nilipoongea nao walilalamikia mfumo kuwa ni mbovu, hivyo fanyieni kazi," alisema.

Waziri huyo alisema kwa kiasi kikubwa Idara ya Uhamiaji inajitahidi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hivyo kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi, lakini lengo la serikali ni kumaliza malalamiko hayo.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeweka msisitizo kwenye kuhudumia wananchi, maagizo yanayotakiwa kutekelezwa na taasisi na idara zote za serikali bila mzaha, hivyo Uhamiaji waandae mpango kazi wa kubadili mfumo wa ukusanyaji maduhuli.

"Wakati tulionao, mifumo kama hii inatakiwa iwe ya kielektroniki na siyo analogia kama huu mnaoutumia. Kwa hiyo andaeni mpango kazi tujue kama unahitaji bajeti ya serikali au mbia ili mfumo wa kisasa ufungwe hapa, kazi ziende haraka haraka.

"Mfumo wa malipo ya kielektroniki utawarahisishia kazi, utapunguza mlundikano wa watu kwenye ofisi zetu na pia utakusanya fedha za serikali vizuri kwa kuziba mianya ya upotevu," alisema Waziri Mwigulu.

Akizungumzia juu ya maslahi ya watumishi wa idara hiyo, alisema ni haki ya kila mtumishi kupata maslahi yake kwa wakati kwa mujibu wa sheria bila ubaguzi, huku pia akihoji sababu za baadhi ya askari wa Uhamiaji kutokulipwa mishahara yao ya Oktoba.

"Niliulizwa swali kwenye moja ya vikao vya bunge lililoisha juzi, kuwa kuna vijana wameajiriwa Septemba, mwaka huu, kwenye Idara ya Uhamiaji, lakini hawajalipwa mshahara mpaka sasa, nini tatizo?" Alihoji.

Akijibu swali hilo, Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Utumishi, Mulegi Majogoro, alisema taarifa za vijana hao, hususan za vyeti vya kuzaliwa na taaluma zilikuwa na matatizo, hivyo zilikataliwa na mfumo.

"Waziri tatizo lilikuwa kwenye vyeti vya waajiriwa, walipoajiriwa tu Septemba 9, wote 297, tulikusanya taarifa zao ili kupeleka utumishi, lakini kule fomu 181, ndizo hazikuwa na makosa. Zingine zilikataliwa kwa sababu ya taarifa kupishana, ikabidi tuwatafute vijana hao wathibitishe taarifa zao.

"Muda huo uliotumika tayari haukuwa rafiki kwa taarifa zao halali kuingizwa kwenye mfumo wa ulipaji mishahara, hivyo hawakuwemo Oktoba, lakini Novemba watalipwa wote," alisema.

Kauli hiyo ilipokelewa na Mwigulu kwa swali lingine lililohoji kuhusu malalamiko mengine ya uwepo wa watumishi waliopandishwa madaraja na vyeo, lakini bado wanalipwa mishahara kiwango cha zamani.

Swali hilo pia lilijibiwa na ofisa huyo, ambaye alisema kwenye kitengo chao wako 10 na kwamba, wametekeleza majukumu yao, hivyo wanasubiri mabadiliko yafanywe na mamlaka zingine za malipo.

Kutokana na majibu hayo, Waziri Mwigulu alisema kitengo hicho hakiwajali watumishi na kwamba, wanatakiwa kufika ofisini kwake leo, saa mbili asubuhi bila kukosa ili wampe ufafanuzi wa baadhi ya mambo.

"Nyie mnafanya utani, mnawaonea askari kwa sababu hawana uwezo wa kuandamana barabarani kudai haki zao, mtu kaajiriwa yuko porini huko, halafu unamnyima mshahara ataishije?" Alihoji.
 
Kuhusu wahamiaji haramu, Waziri huyo alisema Idara ya Uhamiaji wanalo jukumu kubwa la kudhibiti wimbi hilo, ambalo linaenea kwa kasi maeneo mbalimbali duniani kwa siku za hivi karibuni.

Alisema kwenye vituo na ofisi zote za Uhamiaji, hususan mipakani, nguvu iongezwe ili ukaguzi uwe wa ufanisi zaidi ya ilivyo sasa kwa sababu ndiko wanakopitia.

Awali, Kamishna wa Utawala na Fedha wa Uhamiaji, Abbas Irovya, akisoma taarifa ya utendaji kwa waziri huyo, alisema licha ya changamoto walizonazo kwa kipindi cha kuanzia Novemba mwaka jana, wamekamata wahamiaji haramu 23,562.

Alisema idara hiyo inaishukuru serikali kwa kuwarahisishia kazi, hasa kutokana na marekebisho ya sheria mbalimbali, ikiwemo ya kutaifisha gari litakalohusika kwenye usafirishaji wa wahamiaji haramu.

Irovya alisema kwa kutumia ofisi zao 47, zilizoko nchi nzima, wataendelea kufanya kazi kwa bidii, ikiwa ni pamoja na kukusanya maduhuli stahiki ya serikali.

Alisema kwa kutumia fedha zilizotengwa kwenye bajeti, idara hiyo inatekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi, viongozi na kuendesha kiwanda cha kutengenezea nyaraka za kusafiria.      

Katika taarifa hiyo, alisema Uhamiaji imeendelea kuhudumia wateja wake kwa ufanisi, ambapo tangu Novemba, mwaka jana, wametoa nyaraka za kusafiria (pasipoti) 86,645.
   
Alitoa ombi kwa serikali kuongeza idadi ya rasilimali watu kwenye idara hiyo, kutokana na idadi ya watumishi 2,900, kuwa ndogo kwenye uhitaji wa watumishi takriban 10,000, kulingana na kazi zilizopo kwenye ofisi za idara hiyo.
 
Waziri Mwigulu baada ya kumaliza mkutano huo maalumu na watumishi askari na wale wa kada za kiraia wa Idara ya Uhamiaji, alitembelea miradi ya idara hiyo iliyoko eneo la Mtoni Kijichi, ikiwemo kiwanda cha kuchapishia pasipoti.

No comments:

Post a Comment