Friday 25 November 2016

SHIRIKA LA POSTA LAWATANGAZIA KIAMA WABADHIRIFU

BODI  ya Wakururugenzi ya Shirika la Posta, imetangaza kiama kwa watumishi wake baada ya kubaini ubadhilifu mkubwa wa mali zake.

Aidha, imeeleza kushangazwa na watendaji wasio wazalendo, ambao wanaingia mikataba ya  hasara na wizi, ikiwemo wa sh. bilioni tatu wa mafuta kwa magari mabovu.

Bodi hiyo imewataka wadaiwa wake, ambao ni serikali na sekta binafsi wanaodaiwa zaidi ya   sh. bilioni nane, kulipa haraka iwezekanavyo kwa kuwa shirika libakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha.

Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Harun Kondo, alisema kutokana na utendaji mbovu wa watumishi wake, wameona haja ya kutiliana saini mkataba wa utendaji kazi kati ya bodi na menejimenti.

Kondo alisema baada ya mkataba huo, bodi imeielekeza menejimenti kuchukua hatua  stahiki kwa kada zote za wafanyakazi.

"Shirika lina watumishi 1,050, lakini baadhi yao wanafanya kazi kwa mazoea, hivyo ni lazima kusimamia uwajibikaji wa viongozi na watumishi,"alisema.

Alisema bodi hiyo imetoa maelekezo kuhakikisha ngazi zote zinaingia katika mkataba huo.

Alisema shirika kwa kushirikiana na Kampuni ya BICO, limefanya utafiti wa ukaguzi wa rasilimali watu, mapitio ya muundo wa shirika na upimo wa kazi kwa lengo la kuboresha mifumo ya kazi

"Utafiti huo umebaini watumishi wengi hawana fuzu stahiki na wengine umri  ni mkubwa, inabidi kupunguzwa,"alisema Kondo.

Alisema bodi hiyo haikubaliani na utendaji wa mazoea, hivyo kila mmoja awajibike kwa kuwa shirika hilo ni la umma na ni mali ya wananchi.

Kondo alisema hatawavumilia wenye kuficha maradhi ya watendaji wabovu, wanaosababishia shirika hasara, hususani wanaohalalisha wizi ikiwemo katika  mikataba ya nyumba za shirika.

"Haiwezekani hii hasara ya sh. bilioni zaidi ya tatu ya mafuta magari yake yapo karakana kwa miezi 18, hayatumika, imekuaje yanajazwa mafuta na ipo mikataba mibovu ya nyumba,"alisema.

Alisema kati ya mikataba mibovu ni pamoja na jengo  la ghorofa tatu lililoko Ubungo, ambalo linapangishwa kwa sh. 600,000, na mpangaji anajipangia kuwa amefanya ukarabati wa sh. milioni 400, hivyo hatalipa kodi kwa muda anaoutaka.

Kondo alisema kutokana na hali hiyo, ipo haja kupima utendaji kwa kila mfanyakazi na kuboresha mfumo wa TEHAMA.

No comments:

Post a Comment