WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amefuta posho zote zinazotolewa kwenye vikao vinavyoitishwa na Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha, Majaliwa ametoa siku tatu kwa watumishi 10, ambao walitakiwa kuhamia kwenye Wilaya ya Kigamboni, lakini wanaendelea kung’ang’ania wilayani Temeke, kuripoti mara moja.
Hatua hiyo imetokana na ombi lililotolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Happi, ambaye aliiomba serikali kufuta posho hizo na fedha zake zielekezwe kwenye shughuli za maendeleo.
Happi alisema halmashauri zote mkoani Dar es Salaam, zinalipana sh. bilioni 4.5, kwa ajili ya posho ya vikao kwa mwaka.
“Waziri Mkuu kwa kupitia serikali, tunaomba posho hizi zielekezwe katika shughuli za elimu na maendeleo ya jamii kwa sababu ni nyingi sana,” alisema.
Alitoa kauli hiyo jana, kwenye ziara ya siku moja ya kukutana na kuzungumza na watumishi, wadau na wananchi wa wilaya ya Kigamboni.
Alisema Halmashauri ya Kinondoni kwa mwaka, inatumia sh. bilioni 2.2, kwa ajili ya semina na mafunzo, posho na vitafunio.
Aliongeza kuwa Ilala kwa mwaka inatumia fedha za ‘bites’ na kuchochea maendeleo kwa diwani sh. milioni 400 huku Temeke ikitumia sh. milioni 186, kwa mwaka.
“Kigamboni posho ya kuchochea maendeleo ya kata kwa madiwani ni sh. milioni 54, kwa mwaka huku Ubungo sh. milioni 660 hutumika kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya madiwani na ‘bites’ sh. milioni 300,” alisema.
Kutokana na matumizi hayo ya fedha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema anazifuta posho zote na kuwataka wakurugenzi hao kuzingatia tamko hilo.
“Mkurugenzi ukiruhusu hili liendelee, unajipa nafasi ya kuendelea wewe kutokuwepo,” alisema.
Kuhusu watumishi, ambao hawajaripoti kazini, aliwataka kufanya hivyo ndani ya siku tatu, baada ya hapo watakuwa wamejifukuzisha kazi.
“Wale watumishi 10, ambao hawajaripoti kazini waje kazini, natoa siku tatu tu, leo, kesho na keshokutwa, zaidi ya hapo hawana kazi.
“Mbona nyie mmeripoti kwa nini wao washindwe na wanaendelea kung’ang’ania Temeke? Kuna nini huko? Natoa siku tatu tu,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alimtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kumwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, kuhusu watumishi hao ambao hawajaripoti kazini hapo.
Mbali na hilo, Majaliwa aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa bidii na kufuata maelekezo yaliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli.
“Kila mtumishi ni lazima ajue wajibu wake wa kazi na kufuata maelekezo na kuyatekeleza. Unachotakiwa ni kujirekebisha na kufuata matakwa ya kiongozi wa nchi,” alisema.
Aidha, aliwataka watumishi hao kutoa majibu ya kuridhisha kwa wananchi, ambao wanakwenda ofisini hapo kwa ajili ya kutaka msaada.
“Toeni huduma bila upendeleo, bila kujali itikadi, dini wala kabila. Wasaidieni wananchi kufafanua mambo yote yanayohusu sheria,” alisema.
Aliongeza: “Jiepusheni na kauli ya njoo kesho, njoo kesho, hii kauli inatengeneza mianya ya rushwa, msitengeneze mazingira ya kumsumbua mwananchi.”
No comments:
Post a Comment