Tuesday, 3 January 2017
WAFUASI WANANE CHADEMA WABURUZWA KORTINI
MWENYEKITI wa CHADEMA Wilaya ya Karatu, mkoani hapa,Thomas Darabe, amepandishwa kizimbani na wenzake saba, katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, kwa kosa la uharibifu wa mali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 73,000.
Darabe, ambaye pia ni diwani wa kata ya Barai wilayani humo, alifikishwa mahakamani hapo jana, pamoja na Diwani wa Kata ya Man’gola, Lazaro Immanuel (CCM) na Mwenyekiti wa Jumuia ya Watumiaji Maji Mang’ola, Charles Lameck.
Wengine waliopandishwa kizimbani ni George Pius, Baridi John, Christopher Lameck, Florian Tiofil, Daniel Ninida na Lazaro Emmanuel.
Katika kesi hiyo ya jinai namba tatu ya mwaka 2017, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Adelina Kasalla, alidai mahakamani hapo
mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Bernad Nganga, kuwa
watuhumiwa hao kwa pamoja, waliharibu kwa makusudi mali zenye thamani ya sh. milioni 15, kinyume na kifungu cha 326(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Adelina alidai Desemba 27, mwaka jana, huko wilayani Karatu katika Kijiji cha Kang’det, kwenye chanzo cha maji cha Kang’det, watuhumiwa waliharibu injini aina ya Massey, yenye thamani ya sh. milioni 12, pamoja na pampu ya maji yenye thamani ya sh. 3,000,000, mali ya Daniel Awaki, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) wilaya ya Karatu.
Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Serikali, Adelina alimsomea Mwenyekiti wa Jumuia ya Watumiaji Maji, Lameck, shitaka la pili la kuharibu kwa makusudi kinyume cha sheria, injini ya pampu ya maji aina ya AMEC, yenye thamani ya sh. milioni 30,000,000, mali ya Nawe Hecko. Alidaiwa kutenda kosa hilo Desemba 27, mwaka jana, katika chanzo hicho.
Adelina alidai shitaka la tatu, linalomkabili mwenyekiti huyo ni la uharibifu wa mali, alioutenda Desemba 27, mwaka jana, katika chanzo hicho cha Kang’det, ambapo aliharibu pampu mbili za maji aina ya AMEC, zenye thamani ya sh. milioni 6,000,000, pamoja na kuharibu shamba la vitunguu lenye ukubwa wa ekari saba, vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 49, mali ya Demin Demanya.
Baada ya maelezo hayo, watuhumiwa hao wote kwa pamoja walikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana, ambapo mwenyekiti wa jumuia ya watumia maji, aliachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika, zenye thamani ya sh. milioni 14, kila mmoja.
Aidha, watuhumiwa wengine saba, waliachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili, kwa kila mmoja kutia saini dhamana ya mali yenye thamani ya sh. milioni tano.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jumuia ya Watumia Maji Mang’ola, Charles Lameck, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha na kusomewa mashitaka mawili kwa mahakimu tofauti mahakamani hapo.
Akisomewa shitaka la kwanza, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Devota Msofe na Mwanasheria wa Serikali, Charles Kagirwa, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa la uharibifu wa mfumo wa maji, wenye thamni ya sh. milioni 1.6 na pampu yenye thamani ya sh. 2,000,000 .
Baada ya maelezo hayo, mtuhumiwa alikana shitaka hilo na kuachiwa kwa dhamna ya sh. 5,000,000.
Katika shitaka la pili, Mwanasheria Kagirwa, mbele ya Hakimu Patricia Kisinda, alidai mahakamani hapo kwamba, Desemba 28, mwaka jana, mtuhumiwa alitenda kosa la uharibifu wa pampu ya maji yenye thamani ya sh. milioni 3,000,000 na bomba la maji, lenye thamani ya sh. 448,000, kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa alikana shitaka hilo na kuachiwa kwa dhamana ya sh. milioni 5,000,000.
Watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 29, mwaka jana na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Jijini hapa, ambako walikosa dhamana hadi walipofikishwa mahakamani hapo, ambapo watano walirudishwa rumande.
Kesi zote zimeahirishwa hadi Januari 16, mwaka huu, ambapo zitatajwa tena kutokana na upelelezi wa mashauri hayo kutokamilika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment