Wednesday, 4 January 2017

MIL. 950/ ZA FIDIA CCM HATARINI KUTAFUNWA

BAADHI ya watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, wapo kwenye mpango mchafu wa kutaka kujipatia fedha za fidia za Chama Cha Mapinduzi (CCM) sh. milioni 950, kinyemela.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, watendaji hao katika ngazi mbalimbali za uongozi, wamekuwa wakizuia kufanyika kwa malipo hayo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Malipo hayo yanatakiwa yafanywe na Manipaa ya Temeke kwa CCM Tawi la Mivinjeni, kwa ajili ya kutwaa kiwanja namba 228 Kitalu K, Kurasini, ambacho kilikuwa kinamilikiwa na tawi hilo.

Ilielezwa kuwa CCM Tawi la Mivinjeni, ilipata kiwanja hicho tangu mwaka 1986 na mwaka 1992, ilianza kukiendeleza kwa kujenga ofisi ya tawi na mabanda ya biashara.

Tangu kipindi hicho, CCM tawi la Mivinjeni ilikuwa inalipa kodi ya majengo kwa Manispaa ya Temeke, huku pia manispaa imekuwa ikiwatambua kuwa ndio wamiliki halali wa eneo na ndio maana walikuwa wanaandikiwa barua za kukumbushiwa kodi za majengo.

Kiwanja hicho ni miongoni mwa viwanja vilivyotwaliwa na serikali kupitia Halmashauri ya Temeke kwa barua Kumb. Na MD/TMC/F.15/6/77 ya Desemba 12, 2014, ambayo ina orodha na wananchi wanaopaswa kulipwa fidia, ikiwemo CCM Tawi la Mivinjeni, ambao walitakiwa kulipwa sh. milioni 950.

Hata hivyo, taarifa zaidi zilieleza kuwa, kabla ya malipo hayo kufanyika, kulijitokeza msuguano baina ya CCM Tawi la Mivinjeni na wapangaji, ambapo kulifunguliwa shauri namba 197/2007 katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Temeke dhidi ya wapangaji hao, ambapo baadaye CCM Tawi la Mivinjeni na wapangaji, walikubaliana kumaliza kesi hiyo ili malipo yafanyike na hukumu ilitolewa na Jaji Sambo. (nakala ya hukumu tunayo).

Ilifahamika zaidi kuwa kabla malipo hayo hayajafanyika, kulijitokeza tatizo lingine baada mmoja wa watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuandika barua Manispaa ya Temeke, Oktoba 19, 2015 yenye kumb. Na. LD 163696/106, kuzuia malipo hayo huku akidai kiwanja hicho kilimilikwisha kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mtendaji huyo katika barua yake, hakuambatanisha nyaraka zozote kama uthibitisho kuwa mmiliki halali wa kiwanja hicho, ambapo baadae alitoa maelezo kuwa eneo hilo limepita reli.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Yamungu Kayandabila, aliagiza kushughulikiwa kwa mgogoro huo na kufikiwa makubaliano ili kulipwa kwa fidia kwa mtu stahiki.

Hata hivyo, katika kikao kilichoitishwa na Naibu Katibu Mkuu ili kulimaliza suala hilo, kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida na Katibu wa CCM, Tawi la Mivinjeni, Otaigo Marwa huku TRC wakienda watumishi wengine, ambao walidai wamewakilisha uongozi.

Taarifa zaidi zilidai kuwa, kikao hicho kilishindwa kufikia makubaliano ndipo kikaahirishwa, ambapo baada ya muda watendaji wa wizara walipeleka taarifa kwa Katibu Mkuu, Dk. Kayandabila kuwa, wamekubaliana kuwa CCM imekiachia kiwanja hicho kwa TRC, wakati siyo kweli huku kukiwa hakuna maandishi yoyote ya makubaliano hayo.

Gazeti hili lilipata taarifa kuwa, mchezo huo mchafu unalenga kukitengeneza kiwanja hicho kuwa ni mali ya TRC, ikiwa ni sehemu ya kujipatia kiasi hicho cha fedha cha fidia, ambacho kinasubiriwa kulipwa na Manispaa ya Temeke kwa CCM Tawi la Mivinjeni, ambapo baadhi ya watendaji wamekuwa wakikwamisha malipo hayo halali kwa CCM .

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CCM Tawi la Mivinjeni, Marwa huku akiwataja watendaji hao, alisema wamekuwa wakitoa sababu kadhaa ili kuchukua fedha hizo wakijua kwamba CCM watachoka.

"Huu ni uonevu, leo hii Chama tawala tunafanyiwa hivi, tena huku hata barua ya Katibu Mkuu haijajibiwa, ikiwa imekusanya ushahidi wote, wafanye malipo, hawataki kwa maslahi ya mtu mmoja tu. Tunamuomba Rais Dk. John Magufuli na mwenyekiti wetu wa Chama alisimamie hili na Chama kipate haki yake ya fidia,''alisema Marwa.

Alisema watendaji hao walidiriki kudai kuwa, CCM wamekubali kwamba, kiwanja hicho siyo mali yao, hivyo ile fidia ya fedha ichukuliwe na TRC, halafu wawalipe kiasi chao kwa ajili ya kuendeleza kiwanja hicho, huku kukiwa hakuna makubaliano yeyote yaliyofikiwa kwenye kikao hicho.

"Tulimweleza Katibu Mkuu na yeye akawaita akawaambia haya mliyoandika yametoka wapi? Hawakujibu chochote na Katibu Mkuu alitushauri tuandike barua nyingine ya malalamiko na kukana hayo makubaliano, ambapo tumetekeleza yote,"alisema.

Alisema mpango uliopo ni kutengeneza mgogoro mwingine ili waweze kujipatia fedha, kwa kuwa wamekuwa wakiwaeleza kuwa, hiyo fedha ichukuliwe na TRC na wao wawalipe fidia ya majengo na wakati mwingine kudai kuwa, eneo hilo ni la ujenzi wa reli, lakini wakiombwa
uthibitisho wa hayo wanayosema, hawana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Nassib Mbaga, alisema suala hilo analifahamu na tangu alipoanza kazi kwenye manispaa hiyo, amelifanyia kazi na kubaini ukweli kuwa, kiwanja hicho ni mali ya CCM Tawi la Mivinjeni na anachosubiri ni kufanya malipo tu ingawa alisema kuna watu wanafanya ujanja ujanja.

"Ofisi yangu haizuii malipo hayo, hata leo mie naweza kulipa, tena nimewaambia watu wa CCM na hata Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam anafahamu, nilimpigia simu na kumweleza awasaidie watu wake wa CCM Tawi la Mivinjeni huko wizarani kwa kuwa nyaraka walizokuwa nazo zinaonyesha ni mali yao, kinachofanyika ni ujanja ujanja tu, kwani mali ni ya Chama,''alisema.

Mbaga alisema baada ya muda, alisikia kuwa tayari kuna kikao kimefanyika wizarani, hivyo anachosubiri ni mrejesho wa kikao hicho.

No comments:

Post a Comment