Wednesday, 4 January 2017
SERIKALI HAIKURUPUKI KUTOA MAAMUZI- POLEPOLE
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, amesema wananchi wanapaswa kupuuza uzushi unaodai kuwa, serikali inakurupuka kuchukua uamuzi wa jambo lolote kwani uamuzi wowote unaofanywa na serikali, umepangwa kufanyika kwa maslahi ya Watanzania.
Amesema serikali kupitia CCM, inaweka misingi kwa watumishi wa umma kufahamu kuwa, uongozi ni dhamana hivyo haitokuwa na msamaha dhidi ya vitendo vyovyote vya ubadhirifu na rushwa.
Polepole alibainisha kuwa, dhamira ya mabadiliko ndani ya CCM, imejikita katika kukirudisha Chama kwenye misingi iliyosababisha kuanzishwa kwake, ambayo imeainishwa kikatiba.
Aliongeza kuwa serikali imeweka misingi ya kisheria kwa watu wanaojihusisha dhidi ya vitendo vya ya ufisadi, washughulikiwe mahakamani ili haki za Watanzania ziweze kupatikana.
Akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, juzi usiku, Polepole alisema kila kitu kinachofanywa na serikali kimepangwa na kipo kimaandishi, hivyo wananchi wanapaswa kupuuza uzushi unaodai serikali inakurupuka katika kufanya maamuzi.
“Tunayo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, inayoainisha kuwa, tunataka kujenga uchumi utakaotupeleka kwenye uchumi madhubuti wa kati, unaolenga kuondoa umasikini kwenye jamii kwa kujikita kwenye uchumi wa viwanda, utakaoongeza ajira na uzalishaji mkubwa wa bidhaa zitakazotumika ndani na nje ya nchi.
“Dira hiyo ina mpango wa kati, ambao kwa namna ya pekee, umeeleza nyanja mbalimbali katika kufikia uchumi wa viwanda. Kabla ya kuwa na viwanda imebainishwa kuwa, mazingira ambayo lazima yatengenezwe ni pamoja na kuwepo kwa umeme wa uhakika,”alifafanua Polepole.
Alisema serikali ya CCM imefaulu kwa kiasi kikubwa mpaka sasa kutekeleza mpango huo kwa kuwaleta wawekezaji kwenye masuala ya gesi, ambayo imeanza kutumika kwenye viwanda vya uzalishaji saruji na vinywaji.
“Kuna bomba kubwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, kuna mabwawa ya maji yanayoleta ongezeko kubwa la umeme na kuufanya uwe wa kutosha na wa ziada. Uchumi wa viwanda unahitaji umeme wa uhakika kwa matumizi na uzalishaji,” alibainisha.
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, alisema rais kwa mamlaka aliyopewa na Katiba, anayo mamlaka ya kurekebisha na kuweka, yale ambayo wananchi wanayataka na hicho ndicho anachokifanya kwa sasa hadi nchi itakapokuwa imekaa sawa.
Alisisitiza kuwa itakapofika wakati ambao vyama vya siasa vitafanya siasa za kistaarabu na za kuheshimiana, katika kipindi hicho suala la katiba linaweza kuzungumzwa kwa lugha moja.
“Ukiona vyama vya siasa vinadai katiba kuliko wananchi, hapo tunageuza katiba kuwa jambo la kisiasa. Katiba ni jambo la wananchi ndio maana serikali imeamua kudumbukiza kwenye suala la utendaji mambo yote yaliyosemwa kwenye maoni ya wananchi.
“Chama kimeishauri serikali kuanza kuwapatia Watanzania utamu wa lile linalokuja mbele kabla halijafika, hivyo kipaumbele pekee ambacho serikali kupitia maelekezo ya CCM, imeamua kuanza nayo ni kwenye kutendea kazi maoni yaliyotolewa na wananchi katika mchakato wa katiba mpya,” alisema.
Akizungumzia kuhusu maadili na miiko kwa viongozi, Polepole alisema kiongozi wa umma akishateuliwa, mbali na kiapo anachoapa mbele ya rais, ataapa tena ahadi ya uadilifu ya kiongozi wa umma.
Alisema kiapo hicho kimejikita katika misingi ya uwajibikaji, uaminifu pamoja na kusikiliza wananchi.
Polepole aliwataka wabunge wa CCM, kufuata maelekezo ya Chama yaliyoagiza kila mbunge akae kwenye jimbo lake na kufanya siasa za kuhamasisha wananchi kufanya kazi za maendeleo.
“Ikumbukwe kuwa, Chama kimeamua kufanya mageuzi makubwa ambayo yanarudisha kwa wanachama. Mageuzi haya yanakifanya Chama kujihusisha na shida za wanachama, yanatengeneza mfumo wa Chama, aina ya viongozi na mfumo mzima wa uongozi na utawala, ambao unasikiliza watu, wananchi pamoja na wanachama katika yale yote ambayo wanataka kuyaona yamefanyiwa kazi na serikali,"alisisitiza.
Pia, alieleza namna ambavyo serikali kupitia maelekezo ya CCM, inavyotilia mkazo suala la ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge), ambapo fedha zimeshakusanywa ili ujenzi huo uanze haraka.
Alisema badala ya kutumia usafiri wa maroli, ambayo kwa kawaida usafirishaji wake unagharimu fedha nyingi, kutakuwa na uwezekano wa kusafirisha mizigo mikubwa zaidi kwa wakati mmoja na gharama nafuu kwa kutumia njia ya reli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment