Wednesday, 18 January 2017

TAHARUKI JENEZA KUBEBWA TUPU MWILI KUSAHAULIKA


MWILI wa marehemu kusahaulika ndani, waombolezaji kubeba jeneza tupu na kwenda kuzika, kisha kurudi nyumbani na kuukuta mwili juu ya kitanda ulipoachwa, kumeibua taharuki kubwa na sintofahamu jijini Mbeya.

Tukio hilo la aina lake, lilisababisha baadhi ya watu kulihusisha na imani za kishirikina, huku wengine wakifika mbali na kudai marehemu Harun Kyando (9), alifufuka mara tu baada ya kuzikwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula, alisema tukio hilo lilitokea Januari 16, mwaka huu, saa 4:30 asubuhi, eneo la Igoma A, Kata ya Isanga, Tarafa ya Sisimba, jijini Mbeya.

Lukula alisema polisi walipokea taarifa kwamba, maiti iliyokwenda kuzikwa makaburi ya zamani ya Isanga, jijini Mbeya, imekutwa tena nyumbani, ndani ya chumbani ikiwa kwenye godoro.

“Tulifuatilia tukio hilo na kubaini Januari 16, mwaka huu, saa 1:00 asubuhi, muosha magari aitwaye Jailo Kyando (36) na mkewe Anna Elieza (32), waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa kwanza, Harun amefariki dunia akiwa amelala,” alisema.

Aliongeza kuwa, taarifa za awali zinadai marehemu Harun, tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa, hali iliyosababisha kuishi nyumbani pasipo kusoma.

Lukula alisema kufuatia kifo hicho, msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika, ambapo saa 6:00 mchana, jeneza lililetwa msibani na kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu.

“Mwili ulikuwa umeviringishwa ndani ya blanketi na kulazwa chini kwenye godoro. Baada ya maombi yaliyoongozwa na walokole waitwao, Bonde la Baraka, vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha jeneza kuzikwa,” alisema Lukula.
  
Alisema waombolezaji waliporudi nyumbani, walitaharuki kuona mwili wa marehemu Harun, ukiwa chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.

Aliongeza kuwa taarifa hizo zilifikishwa kituo cha polisi, ambapo mara moja walikwenda nyumbani hapo na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu, ambao kwa sasa umehifadhiwa Hospitali ya Rufani Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
 
Lukuka alisema taratibu nyingine za mazishi zilifanyika jana na kwamba, hadi sasa bado haijafahamika ni uzembe ama bahati mbaya, iliyosababisha afiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza.

“Vilevile bado haijafahamika kama kulikuwa na hujuma zozote, hivyo upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hili bado unaendelea kufanyika ili kuweza kubaini ukweli kamili ulivyo,” alisema Lukula.

No comments:

Post a Comment