Wednesday, 18 January 2017

MADIWANI WAWILI CHADEMA MBARONI KWA KUTEMBEZA FEDHA MKUTANONI


MADIWANI wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wametiwa mbaroni, wakigawa fedha kwa wananchi na kuvamia mkutano wa kampeni wa CCM, katika kata ya Ngarenanyuki.

Madiwani hao ni wa kata ya Maruvango na Fadhila Urioh wa viti maalumu kata ya Poli.

Katibu wa CCM Wilaya ya Meru, Langael Akyoo, alisema jana kuwa, madiwani hao walivamia mkutano kwa lengo la kugawa fedha, lakini baadhi ya wananchi waliwaona na kutoa taarifa.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, aliwafuata na kuwasihi waondoke katika mkutano huo kwa kuwa haukuwa mkutano wa CHADEMA na kwamba, wao sio wakazi wa kata hiyo, ambapo walikubali na kuondoka.

Langael alisema madiwani hao waliondoka na kwa kuwa walikuwa hawajatimiza lengo lao, walikwenda nyumba ya jirani na kuanza kuita mwananchi mmoja mmoja, lakini baada ya jitihada hizo kugonga mwamba, walirudi mara ya pili wakiwa  na magari mawili yenye bendera za CHADEMA na kuvamia mkutano huo kwa lengo la kumteka mgombea wa CCM.

"Walikuja mara ya kwanza tukawasihi kwa lugha nzuri waondoke na wakaondoka na kwenda nyumba ya jirani kwa ajili ya kuwarubuni wana CCM baada ya kushindwa kufanya hivyo. Walirudi na magari mawili, ambayo waliyaegesha nyuma ya gari la mgombea wetu, Zakaria Nnko na gari jingine waliliweka mbele ya gari ya mgombea kwa lengo ya kumteka," alisema.

Kufuatia hali hiyo, wana CCM na wananchi wengine walifanikiwa kuwadhibiti, ambapo waliwakamata kisha kupelekwa Kituo cha Polisi Usa River kwa mahojiano.

Uchaguzi katika kata ya Ngarenanyuki unarudiwa kutokana na aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Naftali Mbise (CCM, kufariki ghafla baada ya kuanguka kwenye mti nyumbani kwake.

Uchaguzi huo wa udiwani katika kata ya Ngarenanyuki, unatarajiwa kufanyika Januri 22, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment