CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimewataka Watanzania kuwaogopa baadhi ya wanasiasa wanaopita na kuwaambia kuwa watawapelekea chakula cha bure kuwa hao ni waongo na wachonganishi.
"Kiongozi anayekuja na anasema nitaleta chakula cha bure na watu wasifanye kazi, ni bahati mbaya sana. Viongozi wa namna hii tuwapuuze wanafanya makusudi," amesema Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, kwenye ofisi ndogo ya CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.
Aidha, aliwataka wananchi kuwapuuza viongozi wa vyama vya siasa wanaotumia matatizo yao kujinufaisha kisiasa badala ya kuwasaidia.
Polepole pia alisema wananchi wanatakiwa kuwapuuza viongozi wanaotoa maneno ambayo sio sahihi na ya upotoshaji.
Alisema vyama vya upinzani badala ya kuiga mfano wa CCM wa kuishi kwa misingi ya siasa safi, vimekuwa mstari wa mbele kufanya upotoshaji mkubwa wa kuifitinisha serikali na wananchi wake.
"Wapo watu ambao kwa hakika, furaha yao ni kuona CCM inakwama kama taifa. Malengo yao ni kuona tunashindwa kama taifa. Hii siyo siasa safi, huu sio uongozi bora," alisema.
Alitoa rai kwa Watanzania wenye mapenzi mema na serikali, kuwapuuza viongozi hao wasiokuwa na malengo mema na taifa.
Alisema kutoa kauli za uchochezi zisizokuwa na ukweli wowote, hasara kubwa zitaenda kwa wananchi. "Chama kitasimama imara na wananchi kuhakikisha kinatatua changamoto zao kama ambavyo tumeahidi."
Alivitaka vyama vya upinzani kutoa nafasi kwa CCM ili ipeleke maendeleo kwa Watanzania. Pia alivitaka vyama vya siasa kufanya siasa safi ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
"CCM hatutakwenda mbele kushiriki malumbano yasiyokuwa na tija na hoja. Malumbano ambayo hayana lengo lingine lolote isipokuwa kuchelewesha maendeleo kwa watu wetu.
"Watanzania walitaka viongozi wao wanapowachagua, wakae kwenye majimbo na maeneo yao waliyopewa dhamana, wafanye maendeleo huko, wakawahamasishe wanachama, na sio wanachama wa vyama vyote ni Watanzania," alisema.
Alisema kama Chama, wamewaelekeza wabunge na madiwani wao kuendelea kushirikiana na wananchi katika maeneo ambayo wamepewa dhamana.
Kuhusu taarifa za kuwepo kwa baa la njaa, alisema duniani kote kuna utaratibu unaofahamika bayana kuwa, baa la njaa sio kitu kidogo, ni jambo kubwa ambalo linatakiwa kutangazwa na mkuu wa nchi.
"Katika serikali zote nne zilizopita, hakukujawahi kutokea tatizo hili. Kumekuwa na matatizo ya ukame hapa na pale, sehemu chache za nchi, ambao unaweza kusababisha upungufu wa chakula sehemu moja wapo, hilo siyo baa la njaa," alisema.
Alisema matarajio yake yalikuwa viongozi wote, bila itikadi za vyama, kuwahamasisha Watanzania kufanyakazi kwa bidii, kuhifadhi chakula walichokivuna na wasitumie nafaka zao kwa ajili ya kutengenezea pombe kwa manufaa ya baadaye.
Polepole alisema serikali inazo tani milioni 1.5, ambazo zipo tayari kupelekwa kwenye maeneo, ambayo yanaweza kuwa na uhaba kutokana na hali ya ukame na kuchelewa kwa mvua.
Akizungumzia kuhusu wapinzani kutumia matatizo ya wananchi kama mtaji wa kisiasa, alisema: "CCM tunaamini siasa safi ni siasa ambayo imejengwa kwa misingi ya hoja. Mnapotumia matatizo ya watu kama mtaji wako wa siasa, ni bahati mbaya sana."
Polepole aliwakumbusha Watanzania kuwa, dhamira ya CCM ya kuwaletea maendeleo ipo pale pale kama ambavyo imeainishwa kwenye muelekeo wa sera za Chama, sambamba na Ilani ya Uchaguzi.
"Utekelezaji wa vitu hivi viwili unatupeleka kwenye uchumi wa kati na Tanzania mpya, ambayo pamoja na mambo mengine ni Tanzania ya viwanda," alisema.
No comments:
Post a Comment