WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali inaendelea kufanya mazungumzo na mkandarasi atakayejenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Dodoma ili ndege zinazofanya safari nje ya nchi zianze kutua mkoani humo.
Majaliwa, ambaye alitua uwanja wa ndege wa Dodoma, saa 1:27 asubuhi kwa ndege aina ya Bombadier Q400, alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati alipokuwa akizindua safari mpya za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Alisema Dodoma inayo nafasi ya kujengwa uwanja wa kimataifa Msalato na uliopo sasa utakuwa wa ndege za ndani ya nchi.
"Hapa zitakuja ndege zetu za ATCL, lakini zile za Kenya Airways na zingine zitakuwa zikitua Msalato. Hiyo yote ni faraja. Kuanza kwa safari hizi mkoani zitawezesha wafanyabiashara na wananchi wengine kutoka Dodoma na kwenda katika maeneo mengine kwa urahisi,”alisema.
Majaliwa alisema kuanzishwa kwa safari hizo ni moja ya utekelezaji wa ahadi za Rais, Dk. John Magufuli za kufufua ATCL na kuboresha usafiri wa anga nchini.
“Jambo hili linakamilisha ndoto ya rais wetu. Moja ya ahadi kubwa za rais kwenye kampeni ya mwaka 2015, ilikuwa kuboresha shirika la ndege ili liweze kutoa huduma bora na kwa bei nafuu kwenye viwanja vyetu vya ndege,”alisema.
Aliongeza: "Kutua kwa ndege hii Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kuboresha usafiri kwa gharama nafuu kuja Dodoma. Tukio hili ni mwendelezo wa uboreshaji wa makao makuu ya nchi na mnakumbuka tulizindua ujenzi wa njia ya kutua na kurukia ndege.
Ni wajibu kwa wana- Dodoma kutangaza fursa zilizopo. Jambo hili kwetu ni muhimu na linakamilisha ndoto ya rais."
Gharama za safari ya ndege ya ATCL kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, itakuwa sh. 165,000, kwenda pekee yake na sh. 299,000 kwenda na kurudi.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali ya CCM itaendelea kuongeza viwanja vya ndege na kwa sasa shirika hilo linatua kwenye viwanja vingi vya ndege nchini, vikiwemo Arusha, KIA, Mwanza, Kagera, Kigoma, Zanzibar na baadaye itafika Ruvuma na Mtwara.
"Safari hizo zitaongezeka na tunatarajia kuanza kukarabati na kujenga viwanja vipya na vitaimarishwa viwanja vingine ili ndege ziweze kutua," alisema.
Aliongeza kuwa kuna ndege inakuja Juni, mwaka huu, ambayo itaongeza utoaji huduma na ubora wa usafirishaji wa ndege Tanzania.
Kuhusu uwanja wa ndege uliopo, alisema kwa sasa serikali itaendelea kuuboresha kwa kuupanua, ambapo hivi sasa wanamalizia kulipa fidia ili kuongeza ukubwa wa uwanja huo, ili uwe na uwezo wa kutua ndege kubwa zaidi.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema serikali imefanya jambo la muhimu kwa mkoa wa Dodoma, ambalo limeweka historia mpya na kutoa wito kwa wakazi wa Dodoma, kutumia vizuri fursa hiyo ya safari za ndege za ATCL kwa kuwa utawawezesha kusafiri kwa muda mfupi.
“Kwa kweli tumerahisishiwa usafiri tofauti na awali ukipanda basi lisimame Mbande, Kibaigwa kutwa nzima barabarani sasa ni saa moja tu upo mjini,”alisema Ndugai.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATCL, Kapten Richard Shaid alisema: “Hivi karibuni tunaanza kwenda nchi jirani. Mwakani tutapata ndege nyingine kubwa itakayokuwa inafanya safari za masafa ya kati na mbali."
Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Korosso, alisema hivi karibuni wanatarajia kuanzisha safari za kwenda katika miji ya Tabora, Songea, Mtwara, Mpanda, Mafia na Jiji la Tanga.
Akizungumzia kuhusu safari za Dodoma, alisema zitafanyika mara mbili kwa wiki, siku ya Ijumaa na Jumatatu, huku akisema wanatarajia kuongeza safari hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment