Wednesday, 8 February 2017

SITAKUBALI TANESCO IPANDISHE BEI YA UMEME



Na: Lilian Lundo – MAELEZO - Dodoma

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema kuwa msimamo wake juu ya  Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco)
kutopandisha gharama za umeme kwa wateja wake upo palepale.

Prof. Muhongo ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja
zilizowasilishwa na wabunge  juu ya zuio la upandishaji bei ya umeme kwa shirika hilo wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya shughuli za Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika kipindi cha mwaka  2016/2017.

“Haiwezekani wakapandisha bei ya umeme wakati kuna watu ndani ya Shirika wanamiliki hadi hoteli nne, wakijaza lita 20 za mafuta  katika magari wanaandika lita 50 na kila
mwisho wa mwaka wanagawana milioni 50 kama ‘bonus’,” alifafanua Prof. Muhongo.

Ameendelea kwa kusema kuwa Shirika hilo linadaiwa kiasi cha shilingi Bil. 820, katika deni
hilo kiasi cha shilingi Bil.320 bado hazijachambuliwa. Hivyo shirika hilo
haliwezi kujiamulia kupandisha gharama ya umeme wakati huo huo wakiwa bado hawajachambua baadhi ya madeni yao.

Aidha Prof. Muhongo amesema kuwa, Shirika hilo linahitaji kiasi cha Dola Bil. 12 kwa
ajili ya uwekezaji ili ifikapo mwaka 2020 kiasi cha Mg 5000 za umeme ziweze
kuzalishwa.

Hata hivyo, Prof. Muhongo amesema amekwisha anza kufanya mazungumzo na Benki ya
Dunia ili kuona kama wataweza kufadhili kiasi hicho cha fedha ili kiweze kuwekezwa
katika Shirika hilo.

Aliendelea kwa kusema kuwa Shirika hilo linahitaji mabadiliko ya hali ya juu ili kulifanya
kuwa la kisasa na kuendana na dhima ya nchi ya  uchumi wa viwanda ambao kwa asilimia kubwa unahitaji nishati hiyo ya umeme.

No comments:

Post a Comment