Wednesday, 8 February 2017

KOMREDI KINANA KUONGOZA MAZISHI YA VIONGOZI WA CCM KILIMANJARO


Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ataongoza mazishi ya viongozi wa CCM, waliofariki juzi, kwa ajali ya gari wakati wakitoka kwenye maadhimisho
ya miaka 40 ya CCM, mkoani Kilimanjaro.

"Misiba hii ni mikubwa sana na yenye kuhuzunisha, kwa hiyo nitakiwakilisha Chama, katika mazishi yote ya viongozi wetu hawa kuonesha jinsi walivyokuwa muhimu kwa Chama", amesema Kinana wakati
akisafiri kutoka Mjini Dodoma kwenda Arusha ambako atalala na kesho kwenda mkoani Kilimanjaro kuanza kuongoza mazishi hayo.

Kulingana na taratibu ilizopatiwa ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM kutoka CCM mkoa wa Kilimanjaro, mazishi ya viongozi hao yatafanyika kwa siku tatu tofauti kuanzia kesho ambapo Mjumbe wa NEC wilaya ya Same, marehem Ally Mbaga atazikwa Usangi, Mwanga kesho  Februari 8, 2017 kuanzia saa tisa alasiri.

Taarifa ya taratibu hizo imesema, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (VCCM) Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Anold Swai, atazikwa Masama Mashariki katika kijiji cha Mboyera, Februari 10, 2017, kuanzia saa 8 mchana na aliyekuwa Katibu wa Hamasa wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Mkoa wa Kilimanjaro, Edwin Msele atazikwa eneo la Ukaoni Moshi Vijijini Februari 11, 2017 kuanzia saa tisa alasiri.

Kulingana na taarifa hiyo ya taratibu za mazishi ya viongozi hao, mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT Tawi la Chuo Kikuu cha Ushirika (Moshi) Anastazia Mslamsha, utaagwa kesho Februari 9, 2017, kuanzia asubuhi kwenye Chuo hicho na baadaye kwenda kuzikwa Rombo siku hiyo hiyo alasiri.

Katika ajali hiyo, watu saba wakiwemo viongozi hao na wanachama wanne wa CCM, walikufa baada ya gari aina ya Toyota Hilux walilokuwemo kugongwa kwa nyuma na gari la mizigo la aina Fuso, lililokosa breki katika eneo la Mwika, Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro, siku ya Jumapili ya Februari 5,  2017.

Viongozi na wanachama hao walikuwa wakitoka katika kutekeleza majukumu ya Chama ya Maadhimisho ya Miaka 40 ya Kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kimkoa Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment