Wednesday, 8 February 2017

WASANII 13 WANAOTUHUMIWA KUTUMIA DAWA ZA KULEVYA WAWEKWA CHINI YA UANGALIZI WA POLISI KWA MWAKA MMOJA







Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii

Msanii Wema Abraham Sepetu (28), ameendelea kusota rumande huku wasanii wenzake 13 aliokuwa akishikiliwa nao wakiachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuwa chini ya uangalizi wa polisi na mahakama kwa kipindi cha miaka minne.

Miss Tanzania wa mwaka 2006 huyo anaendelea kushikiliwa kwa zaidi ya saa 72 kwa sasa kwa tuhuma za kukutwa msokoto mmoja wa bangi na kusubiri uchunguzi kukamilika. Taarifa kutoka chanzo makini cha habari kinasema Wema anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi na muda wowote wiki hii anaweza kufikishwa mahakamani.

Katika kesi hiyo iliyokuwa  mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam ilisikilizwa na mahakimu wawili ambapo watuhumiwa nane wa mwanzo walipewa dhamana ya milioni kumi (10,000,000) kila mmoja na watakuwa chini ya uangalizi wa polisi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Watuhumiwa hao ni Hamidu Salum Chambuso (Dogo Hamidu), Rajabu Salum, Romeo George Bangura (Romy Jons), Cedou Madigo, Khalid Salum Mohamed (TID), Johana Johanenes Mathysen (Director Joan), Rachael Josephat (Rachel) na Anna Patric Kimario (Tunda).

Mbele ya Hakimu Mkazi  Mhe. Huruma Shahidi washitakiwa walitakiwa kujibu maombi ya waleta maombi (upande wa Jamhuri)  yaliyowasilishwa chini ya kiapo kilichoapwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Dennis Mujumba wa kitengo cha dawa za kulevya.

Sehemu ya kiapo hicho inataja kuwa wajibu maombi hao wanajihusisha na madawa ya kulevya hivyo kutokana na tabia hizo kuwaachia huru katika jamii bila kuwadhibiti kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani zaidi.

Katika maombi hayo, upande wa Jamhuri uliiomba mahakama iwaamuru wajibu maombi (wasanii hao), kuweka dhamana ya kuwa na tabia njema kwa kipindi cha miaka mitatu na kuwaamuru kuripoti katika kituo cha polisi cha kati mara mbili kw  mwezi kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa tabia zao.

Aidha Jamhuri iliiomba mahakama itoe amri yoyote nyingine itakayowafanya wajibu maombi hao kuwa na tabia njema na kuachana na kujihusisha na madawa ya kulevya.

Upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na wakili Albert Msando ulidai kuwa kifungu cha sheria 73B ambacho wasanii hao wameshtakiwa nacho hakuna sehemu inayoonyesha makosa ya uvunjifu wa amani na kwamba mtu anayejihusisha na madawa ya kulevya hawezi kuvunja amani.

Akitoa amri, Hakimu Shahidi amewaamuru wasanii hao kuwa chini ya uangalizi wa mahakama kwa muda wa mwaka mmoja, na pia wametakiwa kuwekewa dhamana ya kiasi cha milioni kumi (10,000,000) kila mmoja na pia wawe chini ya ulinzi wa polisi  ili waweze kujirekebisha,  na iwapo watakiuka watarudishwa mahakamani. 

Wasanii Ahmed Hashim (Petitiman), Said Masoud Linnah (Said Alteza), Nassoro Mohamed Nassoro Bakar Mohamed Khelef na Lulu Abbas Chalangwe (Lulu diva) walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi Cyprian Mkeha.

Katika amri zake, Hakimu Shahidi  aliwataka wasanii hao kuweka dhamana ya kiasi cha shilingi milioni ishirini (20,000,000) kila mmoja na kutojihusisha na makosa ya dawa za kulevya kwa kipindi cha miaka mitatu na wanatakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Kati kwa mwezi mara mbili pamoja na kutakiwa wabadilike na kuacha kabisa matumizi ya dawa hizo.

Hadi Globu ya Jamii inaondoka katika viwanja vya mahakama hiyo, wasanii hao walikuwa wamekamilisha taratibu zote za mahakama na walikuwa wakisubiri kurudishwa polisi kumalizia taratibu kabla hawajaachiwa huru.

No comments:

Post a Comment