Thursday, 9 February 2017
WABUNGE WARIDHIA MAKONDA AITWE NA KUHOJIWA NA BUNGE
Wabunge wamepiga kura ya maazimio ya kuwaita kwenye kamati ya maadili ya Bunge, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kwa madai ya kutoa lugha za kulidhalilisha Bunge.
Awali, wabunge waliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, akubali bunge kujadili kauli za Makonda, aliyetuhumiwa kwa kunukuliwa akiwazungumzia wabunge.
‘Unajua zile ni mbwembwetu, wakati mwingine wale huwa wanachoka na kusinzia hivyo ni lazima wakati mwingine kuwe na watu akili zao zinasaidia kucheka,’ Makonda alikaririwa akisema alipozungumza na wanahabari juzi.
Baadhi ya wabunge wakiwemo Abdallah Ulega, Ester Bulaya, Mwita Waitara pamoja na Joseph Msukuma walisimama kuelezea Bunge namna walivyozipokea taarifa za Makonda huku wakiendelea kushinikiza bunge lizipokee hoja na kutaka kamati ya maadili itekeleze wajibu wake wa kumtaka kufika bungeni kwa ajili ya mahojiano.
Mwingine aliyedaiwa kutoa lugha za kudaiwa kudhalilisha bunge ni Mkuu wa wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti ambae naye anadaiwa kurekodiwa sauti akikashifu utendaji kazi wa bunge , bunge liliafiki ajumuishwe kwenye tuhuma hizo na kuitwa kwenye kamati hiyo ya maadili.
Mwenyekiti wa bunge Andrew Chenge baada ya kuzisikiliza hoja zote za wabunge alitoa nafasi kwa Wabunge kupiga kura za Ndio au Hapana kuruhusu azimio la Watuhumiwa wote kuitwa mbele ya kamati ya maadili ya Bunge ambapo kura zote zilikuwa za Ndio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment