Thursday 9 February 2017

WEMA AACHIWA KWA DHAMANA, AFIKISHWA MAHAKAMANI AKIWA NA TUNDU LISSU





Na Karama Kenyunko,Globu ya Jamii.

Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu imewaachia kwa dhamana msanii maarufu nchini Wema Sepetu na wenzake wawili baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambaye kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni tano.

Baada ya kutimiza masharti hayo, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Thomas Simba aliwataka washitakiwa kuhakikisha hawaruki dhamana waliyotakiwa na kuhakikisha wanafika mahakamani hapo kila wanapohitajika.

Hata hivyo, aliwataka mawakili wa serikali kukamilisha upelelezi haraka ili kesi hiyo ifike mwisho. Mbali na wema washtakiwa wengine ni Angelina Msigwa ambaye ni mfanyakazi wa ndani na Matrida selemani Abas ambaye ni Mkulima.

Wote watatu wanashtakiwa na kosa la kukutwa na kiasi kidogo cha madawa ya kulevya chini ya kifungu cha sheria namba 17 (1)(b) cha sheria inayodhibiti matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, iwapo Wema na wenzake watapatikana na hatia basi watatakiwa kulipa faini isiyozidi sh.laki tano au kwenda jela.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa serikali Nassoro Katuga aliyekuwa akisaidiana na Wakili Pamela Shinyambala walidai kuwa Wema na wenzake watatu walitenda kosa hilo tarehe 4 February mwaka huu, huko nyumbani kwao Kunduchi Ununio.

Ilidaiwa kuwa, siku hiyo walikutwa wakiwa na msokoto mmoja pamoja na vipisi viwili vya banfi vyenye gramu 1.80. Hata hivyo washtakiwa wote wamekana mashtaka.

Akielezea hali ya upelelezi wakili Katuga alidai "mheshimiwa Hakimu, upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika tunasubiri taarifa kutoka kwa Mkemia Mkuu ambayo tunategemea kuipata hivi karibuni".

Hakimu Simba aliwapa washtakiwa masharti ya dhamana ambapo mahakama ilimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakao weka dhamana na milioni tano. Mshtakiwa Wema na Wenzake walitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo February 22 mwaka huu.

Nje ya Mahakama Umati wa watu na wasanii mbali mbali walijaa nje kumlaki Wema akitoka mahakamani baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

No comments:

Post a Comment