Friday, 10 February 2017

WAGANGA WAKUU WA WILAYA ZA MKOA WA TABORA WAAGIZWA KUWAFANYIA UCHUNGUZI WANAUME KUBAINI WASIOFANYIWA TOHARA


Katibu Tawala Mkoa wa Tabora,Dk.Thea Ntala akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na madiwani,watendaji wa Halmashauri ya wilaya pamoja na viongozi wa chama na serikali waliohudhuria mkutano huo wa kawaida wa Baraza la madiwani uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.


KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tabora,amewaagiza waganga wakuu wa wilaya za Mkoa huo kuhakikisha kwamba wanaume wote watakaougua na kulazwa Hospitalini kwa ugonjwa wowote ule,wawaambie kuwa ugonjwa huo unatokana na uchafu unaotoka kwenye
sehemu za siri za mwanaume huyo kutokana na kutofanyiwa tohara.

Katibu Tawala huyo,Dk.Thea Ntala alitoa agizo hilo alipokuwa akiongea na
madiwani pamoja na watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga kwenye
mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo
uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

“Nimewaagiza waganga wakuu wote wa wilaya kuwa mgonjwa yeyote mwanaume akiwepo mheshimiwa diwani,akiwepo mheshimiwa mbunge wakilazwa pale Hospitali awe
anaumwa jino,awe anaumwa sikio,awe anaumwa mkono mwambie hivi hili
tatizo lako linatokana na uchafu unaotoka kwenye sehemu za siri kwa
kutofanyiwa tohara”alisisitiza katibu tawala huyo.

Kwa mujibu wa Dk.Ntala haiwezekani katika Mkoa wa Tabora wakaendelea kukaa na wanaume ambao mpaka sasa bado hawajafanyiwa tohara kwani kuendelea kukaa na watu
wa aina hiyo kunachangia kwa namna moja au nyingine ongezeko la
maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.

“Hatuwezi kukaa Tabora,hatuwezi kukaa na hicho kitu na ndiyo maana ugonjwa huu wa ukimwi unaendelea kutokana na sababu za kuendelea kuwepo kwa watu wasiofanyiwa
tohara,nimewaagiza MADMO,RMO hili nimewaagiza wote Tabora kuhakikisha
wanawafanyia uchunguzi wanaume wote wanaolazwa iwapo wamefanyiwa
tohara”alifafanua huku akiwaacha waliohudhuria mkutano huo wakiangua
kicheko.

Hata hivyo Dk.Ntala alibainisha kwamba hivi sasa baadhi ya wanaume wamekuwa wakihudhuria kwenye semina kupatiwa elimu ya juu ya umuhimu wa kufanyiwa tohara huku wengine wakiamua kwenda kwa hiyari yao kufanyiwa tohara hiyo kwenye maeneo yanayotoa huduma hizo.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa mabusha,Dk.Ntala alitumia fursa hiyo kuwashauri
wanawake kumeza dawa kwani dawa za ugonjwa huo zinatakiwa kumezwa na
wanaume pamoja na wanawake na kuonya dhana potofu iliyojengeka miongoni
mwa jamii ya kuamini kwamba ugonjwa wa mabusha hauwahusu wanawake bali
unawahusu wanaume peke yao.

“Madiwani mnisaidie kwenye mikutano wanawake wanafikiri ukiongelea ugonjwa wa mabusha ni wanaume,aah mwanamke anapata mabusha kwenye matiti yaani badala ya kuwa na saizi ya kawaida kama ya RAS anakuwa na saizi kubwa kama tikitimaji fulani
hivi…sijui kama kuna watu wanapenda magodoro makubwa”alibainisha katibu
huyo tawala.

No comments:

Post a Comment