Friday, 17 March 2017

SIR GEORGE KAHAMA AAGWA NA KUZIKWA DAR









Na Shamimu Nyaki-WHUSM

Serikali imesema itaendelea kuenzi na kuheshimu mchango mkubwa katika kupigania maendeleo na ustawi  wa jamii uliofanywa na  marehemu Sir George Kahama  enzi za uhai wake alipokuwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akitoa salamu za Serikali katika tukio la kumuaga mmoja wa waasisi wa Taifa na Waziri msataafu marehemu Sir Gorge Kahama aliyefariki dunia Machi 12 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Waziri Nape amesema kuwa Sir George Kahama alikuwa kiongozi mahiri na aliyetekeleza majukumu yake kwa ufasaha ambapo alikuwa miongoni mwa viongozi walioanzisha harakati za Serikali za uendelezaji  wa mji wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya  kuimarisha makao makuu ya nchi.

“Marehemu Sir George Kahama tutamuenzi kwa kuendeleza yale mazuri aliyoyafanya katika kuijenga nchi yetu hasa katika ustawi wa jamii na kuimarisha uchumi wa nchi”.Alisema Waziri Nape.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bw. Abdurahaman Kinana amumueleza Sir George Kahama kama kiongozi mahiri katika Chama aliyependa maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla katika weledi wa hali ya juu na alikuwa mchapakazi.

“Sir George Kahama alikuwa mtumishi na kiongozi aliyetukuka  ametuachia hamasa kubwa ya kuwa viongozi bora zaidi na wenye mapenzi na Taifa letu katika kuleta maendeleo.”Alisema Ndugu Kinana.

Marehemu Sir  George Kahama amekuwa Waziri na Kiongozi kabla na Baada ya Uhuru wa Tanzania  Bara kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amezikwa leo Jijini Dar es Salaam na ameacha Mjane na Watoto.

No comments:

Post a Comment