Monday 10 July 2017

HALIMA MDEE ASOMEWA SHITAKA LA KUMTUKANA RAIS MAGUFULI, MALIMA ATINGA TENA KORTINI



Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Halima Mdee, amesomewa shItaka moja la kumtukana Rais John Magufuli, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Halima alisomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, ambapo imeelezwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja pekee.

Katuga alidai kuwa, Julai 3, mwaka huu, katika ofisi za CHADEMA makao makuu, alimtukana Rais Magufuli kwa kumwambia 'anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afunge break.'

Baada ya kusomewa kosa hilo, Halima alikana.Wakili Katuga alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliomba kesi iahirishwe.

Halima alidhaminiwa kwa bondi ya shilingi milioni kumi na wadhamini wawili.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 7, mwaka huu.

Wakati huo huo, mbunge wa zamani wa Mkuranga na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima na dereva wake, Ramadhani Mohammed, leo wamesomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam.

Maelezo hayo, ambayo Malima na dereva wake wameyakana,  yalisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage na Wakili wa Serikali, Ester Martin.

Malima na Ramadhani walikubali maelezo yao binafsi siku ya tukio kwa kukiri walikuwepo Masaki, kukamatwa na kushtakiwa pamoja na kuyakana mashtaka yote yanayowakabili. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 9, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Malima anadaiwa kuwa Mei 15, mwaka huu, katika eneo la Masaki, kwa makusudi alimzuia ofisa wa polisi H.7818 PC ABDU, kufanyakazi yake halali, ambapo anadaiwa kumzuia kufanyakazi yake ya kumkamata Ramadhani Kigwande kwa kosa la kumshambulia Mwita Joseph.

No comments:

Post a Comment