Tuesday 11 July 2017

MAJIPU SASA YANAJITUMBUA YENYEWE-JPM





RAIS Dk. John Magufuli, ametangaza kuhamishia vita ya ufisadi kwenye pembejeo hewa na ukaguzi huo unatafanyika nchi nzima na matokeo yake kuwekwa hadharani.

Alitoa kauli hiyo jana, mjini Chato, mkoani Geita, katika sherehe za kukabidhiwa nyumba 50, za watumishi wa afya zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa.

Rais Dk. Magufuli alisema fedha za ruzuku za mbolea na pembejeo zimekuwa zikipotea bila kuwafikia walengwa.

"Kama patakuwa na mgogoro mkubwa ni katika fedha za pembejeo. Fedha zimekuwa zikigawiwa hata kwa watu ambao wameshakufa," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema wameamua kufanya ukaguzi katika mikoa 11, ambayo madai yalikuwa sh. bilioni 50, lakini walikuta madai halali ni sh. bilioni nane.

"Na wanaohusika wengine ni viongozi wa ndani ya serikali na halmashauri. Hapa hapa Chato, fedha za pembejeo zililiwa shilingi bilioni 1.5. Na siku moja nilimuuliza mama, mbona na wewe upo kwenye orodha, ulichukua pembejeo, ulichukua vocha, akafikiri vocha ni ile anayonunuliwa kuweka kwenye simu," alisema.

Aliongeza: "Mchezo huu upo karibu kila mahali, tunafanya ukaguzi Tanzania nzima, nayo tutayasema hadharani. Kumekuwa na hewa nyingi, hewa TASAF, mishahara, wafanyakazi."

Kutokana na hali hiyo, aliwaomba viongozi wote nchini kushirikiana, ikiwa ni pamoja na kuiga mfano mzuri ulioonyeshwa na Taasisi ya Mkapa katika kusimamia miradi.

"Viongozi wetu wa mikoa, wilaya tusimamie miradi yetu. Watanzania hawa wana matumaini makubwa na serikali yao, wamechoka kukaa wanaonewa kila siku na ndiyo maana serikali yangu ninayoiongoza, nazungumza siku zote kuwa nitakuwa upande wa wananchi, hasa wale wanyonge," alisema.

KUFUTWA KWA TOZO

Akizungumzia kuondolewa na kufutwa kwa tozo, alisema waliondoa na kufuta tozo zaidi ya 80, kwenye kilimo, saba kwenye mifugo na zaidi ya nane kwa wavuvi.

"Kwenye kilimo mtu ulikuwa una debe moja la mpunga, unaambiwa ulipe ushuru. Tumesema sasa hivi, ukitoka na tani moja kutoka wilaya moja kwenda nyingine, hakuna kulipa ushuru. Kama umepakiwa viazi vyako tani moja, hakuna kulipa ushuru, wewe ondoka na mtu wa ushuru asikufuate na yeye alime viazi aone shida yake," alisema.

Rais Magufuli aliongeza:"Serikali haiwezi kufanya biashara na watu maskini, inawaacha matajiri, inaanza kusumbua masikini. Kwa hiyo wakulima fanyeni biashara ili kusudi mjenge maisha yenu."

Pia, alisema kulikuwa na ushuru wa kwato, ambapo ukipeleka ng'ombe mnadani ni lazima uzilipie. "Kwato umeziumba wewe, ukizivalisha njumu ili ng'ombe ilipe kodi."

KUHUSU MADINI

Akizungumzia kuhusu madini, alihoji kwa nini Watanzania wasiwe wawekezaji kwani wanashindwa kununua magreda na kuanza kuchimba.

Kutokana na hali hiyo, aliiagiza Wizara ya Nishati na Madini, kutotoa leseni ya aina yoyote hadi serikali itakapojipanga upya na iwapo itatolewa, nao wataondoka nayo.

"Ni lazima tujipange upya, tuzipitie hizi leseni zote tuweze kufaidi na haya madini yetu, ambayo tumepewa na Mungu. Lazima tulinde rasilimali hizi, tusipofanya hivyo tutabakiziwa mashimo na baadaye matetemeko yatakuwa yanakuja. Hatujazuia watu waje kuchimba, lakini wachimbe na sisi watuachie faida," alisema.

AWAONYA WAKUU WA MIKOA, WILAYA

Kutokana na kuongezwa kwa bajeti ya afya, alitoa wito Kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi nchini, kuhakikisha wanajifunza kutumia vizuri fedha zinazotolewa na serikali.

Alisema tatizo lililopo katika halmashauri nchini ni matumizi mabaya ya fedha za serikali.

"Unaweza ukakuta serikali inahangaika kutafuta hizo fedha, asitokee mtu wa kuzila hizi fedha, dawa zitumwe halafu kila siku mtu akienda hospitalini anaambiwa dawa hakuna. Nawaomba viongozi wenzangu tubadilike, tuhakikishe tumepewa dhamana ya uongozi kwa ajili ya manufaa ya wananchi tunaowaongoza.

"Imekuwa ni kawaida fedha zinapotumwa kwenye halmashauri matatizo yanakuwa ni mengi. Inawezekana tumejijengea utaratibu wa namna hiyo, tuanze kubadilika," alisema. 


AMMWAGIA SIFA MKAPA

Pamoja na hayo, alimshukuru Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kumfundisha kazi na kumnadi kwa wananchi ili aweze kuchaguliwa kuwa mbunge wa Chato mwaka 1995.

"Nakumbuka maeneo yale yaliposimama magari katika uwanja huu (Chato) kwenye mwaka 1995, ulinisimamisha na kuninadi kwa wananchi. Nakumbuka ulikuwa umevaa viatu vyekundu. Ukaniinua ukasema mchagueni huyu, nileteeni huyu.

"Wananchi wa Chato walikusikiliza na wakakuamini na wakanichagua kuwa mbunge. Na kwa mshangao mkubwa, ukaniteua kuwa naibu waziri wa ujenzi. Nilikuwa nakusikia hapa mzee wangu ukisema natakiwa kushukuru, sasa usingenichagua mimi ningejulikanaje," alisema.

Aliongeza: "Unayetakiwa kushukuriwa ni wewe, ninajua ni ukweli Mzee Mkapa huwa hupendi sifa, lakini kwenye hili mimi naomba nikushukuru kwa sababu mimi sikustahili chochote, lakini wewe Mungu alikuongoza na ukanichagua."

Vilevile, alimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye katika kipindi chake, hakusita kumchagua tena kuongoza wizara mbalimbali.

"Namshukuru sana Mzee Kikwete. Kwa hiyo kwangu mimi, ambao mmetengeneza maisha yangu kwenye uongozi ni wewe (Mzee Mkapa) na Mzee Kikwete," alisema.

Pia, aliwashukuru viongozi wa awamu ya kwanza, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na wa awamu ya pili, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ambao wametengeneza mazingira mazuri kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rais Dk. Magufuli aliwashukuru wananchi wa Chato na Watanzania kwa kumpigia kura na kuahidi kuwafanyia kazi kwa nguvu zake zote.

"Namuomba sana Mwenyezi Mungu asinifanye nikawa na kiburi, asinifanye nikasahau nilipotoka. Nilikuwa nauza maziwa na niliokuwa nawauzia najua wengine bado wapo, nimechunga ng'ombe kwa hiyo maisha nayafahamu.

"Na kwa sababu ninayafahamu, ndiyo maana nimeamua kuwasaidia. Watanzania wengi wana maisha ya chini na kwa sababu hiyo sitaki Watanzania wenye maisha ya chini waonewe katika kipindi changu," alisema.

Aliongeza: "Nataka kuwathibitishia Watanzania kuwa tutafanyakazi kwa nguvu zetu zote ili kuhakikisha tunatimiza malengo yenu."

Alimpongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kuwa ni mmoja wa mawaziri, ambao wanafanya kazi kwa nguvu zote kwa sababu kila anapopewa maelekezo anayatekeleza.

"Nilimwambia kwamba gharama za dawa zimekuwa juu sana, hivyo ni lazima zipungue na yeye akatekeleza," alisema.

Kuhusu ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya, alimshukuru Rais mstaafu Mkapa na taasisi yake kwa kujenga nyumba zitakazotumiwa na watumishi hao.

"Namshukuru Mzee Mkapa na taasisi yake kwa kazi kubwa wanayoifanya, tangu waanze wameshajenga nyumba zaidi ya 450, nchini na wameshatumia zaidi ya sh. bilioni 26 katika mikoa 17.

"Wameweza kusomesha zaidi ya madaktari 900.Mzee Mkapa na hili nalo unataka ukatae nisikushukuru kweli? Umeshastaafu urais, ungeweza ukakaa tu na kupumzika na kula pensheni. Una miaka 79, lakini unaonekana kijana, mimi ndio naonekana mzee, lakini upendo wako ulionao kwa Watanzania uliamua hata baada ya kustaafu, unaendelea kuwahudumia," alisema.

Aliongeza: "Ndiyo maana leo (jana), umekuja kuzindua nyumba za mikoa hii mitatu (Simiyu, Geita na Kagera), najua kuna watu wengine watakuwa hawaelewi amejenga nyumba hadi Mtwara na Tanga, sisi tumekuwa wa mwisho mwisho."

Alisema inawezekana kuna baadhi ya watu watageuza maneno wakisema kuwa nyumba zimejengwa kwa Magufuli tu, lakini kumbe zilianzia kujengwa mbali.

"Umejenga hizi nyumba, vituo vya afya na hospitali mbalimbali, ungeweza kukaa tu na kuamua kufanya biashara, kila mgonjwa atakayeingia alipe fedha, lakini unagawa bure," alisema.

Kuhusu serikali ya Japan, alisema inaifadhili Tanzania katika miradi mbalimbali huku ikijenga barabara ya juu 'flyover' ya kwanza maeneo ya TAZARA.

"Kwa hiyo mimi ni ombaomba, nakuachia sasa Kalemani (Naibu Waziri wa Nishati na Madini), nawe uwe ombaomba kama mimi. Nilitimiza wajibu wangu na kwa sasa nitaomba kwa ajili ya Tanzania nzima," alisema.

MKAPA AIPONGEZA SERIKALI

Awali, mgeni rasmi, Rais mstaafu Mkapa, alisema nyumba hizo zilizojengwa na taasisi yake kwa kushirikiana na wizara ya afya, ni kielelezo tosha cha utayari wa serikali kuungana na wadau wa aina zote katika kufikia Dira ya Maendeleo ya 2020.

"Naishukuru kwa dhati serikali yako kuwa na imani na Taasisi ya Mkapa, tangu ilipoasisiwa miaka 11 iliyopita. Nina imani ushirikiano huu utaimarika zaidi chini ya serikali yako, hasa kwa sababu ya kauli mbiu yako ya hapa kazi tu," alisema.

Mkapa alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania unategemea afya bora ya wananchi wake, ambao ndiyo wasimamizi na watekelezaji wa mikakati ya kuinua uchumi wa nchi.

Alisema hakuna budi kila mmoja kujituma na kujikinga na maradhi na kuhakikisha watu wanatumia huduma zinazotolewa na vituo vya afya ipasavyo kwa kufuata masharti, maelekezo na tiba wanazopatiwa na wataalamu.

Pia, alisema anatambua kuwa, Tanzania bado ina uhaba wa wataalamu wa afya, lakini wale wachache waliopewa dhamana ya kutoa huduma hiyo, hawana budi kujituma na kufanyakazi kwa ufanisi na kuheshimu haki za binadamu.

Mbali na hilo, aliwashukuru wananchi wa Chato kwa kumuamini na kumchagua Rais Magufuli ili aweze kuwaongoza.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy alisema utoaji wa huduma za afya nchini unaendelea kuimarika kutokana na msingi mzuri aliouweka Rais mstaafu Mkapa wakati wa utawala wake.

Ummy alisema wakati wa utawala wa Mzee Mkapa, alianzisha Mfuko wa Bima ya Afya, ambao uliwezesha Watanzania kupata huduma hizo bila kikwazo cha fedha.

"Rais mstaafu inabidi utembee kifua mbele kwa sababu asilimia 28 ya Watanzania wanatumia bima ya afya, ingawa hatujafika lengo letu," alisema.

Alisema ili kuendeleza juhudi hizo, serikali ya awamu ya tano itahakikisha kuwa, wakurugenzi wa halmashauri zote, wanawakatia bima au kuwapa vitambulisho vya matibabu wazee wasiokuwa na uwezo.

Pia, alimpongeza Rais mstaafu kwa kushirikiana na serikali na kuhakikisha kuwa huduma za afya nchini zinaimarika.

Kuhusu vituo vya afya, alisema kwa sasa wameongeza vituo vya kutoa huduma kutoka 4,000 hadi 7,200.

Vilevile, alisema nchi imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja na wa chini ya miaka mitano kwa asilimia zaidi ya 50.

Ummy alisema pia wamepunguza udumavu wa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 42 hadi kufikia 34.

Akizungumzia changamoto, alisema kwa sasa wana changamoto itokanayo na vifo vya uzazi, ambapo katika kila wanawake 100,000 wanaojifungua, 556 wanafariki kutokana na uzazi.

Kutokana na hali hiyo, alimshuruku Rais Magufuli kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na kuiongezea bajeti.

MSUKUMA AOMBA MSAADA

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku 'Msukuma', aliiomba serikali itakapolipwa fedha na Kampuni ya Acacia, kuujengea mkoa huo miundombinu ya barabara, hospitali na shule.

Alisema mkoa wa Geita ni tajiri sana kutokana na kuwa na mgodi mkubwa wa dhahabu, lakini uko nyuma kimaendeleo.

"Tunaomba sana Rais na sisi utukumbuke mara mtakapolipwa fedha na Acacia, mtujengee hata barabara, zahanati, shule ili na sisi tufurahie matunda ya kuwa na mgodi," alisema Musukuma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo.


BALOZI WA JAPAN ATOA NENO

Naye Balozi wa Japan nchini, Masharu Yoshida, alisema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania katika ujenzi wa miundombinu pamoja na kutoa msaada katika shule na hospitali.

MBUNGE WA CHATO

Kwa upande wake, Mbunge wa Chato, Dk. Medard Kalemani, aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwajengea nyumba za watumishi wa afya.

Dk. Kalemani, ambaye pia ni Naibu waziri wa Nishati na Madini, alisema nyumba hizo zitawasaidia watumishi waliokuwa wanakaa mbali na vituo vya kutolea huduma za afya.
 

No comments:

Post a Comment