RAIS Dk. John Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison George Mwakyembe, kufuatia
kifo cha mkewe, Linah.
Linah, alifariki usiku wa kuamkia juzi, katika Hospitali ya
Aga Khan, jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika salamu zake, Rais Dk. Magufuli ameelezea kushtushwa na
kusikitishwa na kifo hicho.
Alisema yeye pamoja na familia yake wanaungana na familia ya
Dk. Mwakyembe katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Nakupa pole Dk. Mwakyembe kwa kuondokewa na mkeo mpendwa
Linah, natambua hisia za maumivu ulizonazo wewe na familia nzima, nyote nawaombea
Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu
cha majonzi.
“Namuombea marehemu Linah George Mwakyembe, apumzishwe mahali pema
peponi,”alisema.
Wakati huo huo, Dk. Magufuli jana, alisali Ibada ya Jumapili
ya 15 ya mwaka wa Kanisa, iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Parokia ya
Chato, mkoani Geita na aliendesha hafla ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.
Katika hafla hiyo, Dk. Magufuli, ambaye aliongozana na mkewe
Mama Janeth, alifanikiwa kuchangisha sh. milioni 13, ahadi sh. 920,000, mifuko
ya saruji 33 na malori mawili ya mchanga.
Rais Dk. Magufuli aliwapongeza waumini wa Parokia ya Chato kwa
hatua kubwa waliyopiga katika ujenzi wa Kanisa Kuu la Parokia hiyo na aliwataka
waendelee kujitolea ili kukamilisha hatua ya mwisho ya ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment