NA WILIUM PAUL, HAI
WAKATI bundi akiendelea kukitafuna Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), kutokana na kukimbiwa na viongozi wake, Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kimeitikisa ngome ya mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman
Mbowe, baada ya wanachama zaidi ya 200 kurudisha kadi na kujiunga na CCM.
Wanachama hao walioongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA
katika Kijiji cha Mijongweni, Hasan Hamisi,
walirudisha kadi zao jana na kukabidhiwa za CCM.
Tukio hilo lilitokea katika kikao cha Chama, kilichofanyika
kijijini hapo, wilayani Hai, ikiwa ni
hitimisho la ziara ya Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali
Ngemela Lubinga, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza mbele ya wana-CCM, baada ya kurejesha kadi yak,
Hamisi alisema tangu ashike nafasi hiyo kwa miaka mitano, hakuna faida yoyote
ya maendeleo iliyotekeleza na chama hicho.
Hamisi alisema sababu zilizosababisha aamue kuhamia CCM ni
kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Dk. John Magufuli.
“Nimeamua kurudi CCM baada ya kuvutiwa na kazi nzuri
inayofanywa na Chama Cha Mapinduzi. Wametambua vilio vya wananchi na kuamua
kuvifanyia kazi kwa vitendo bila kujali kipato cha mtu. Wananchi walio na kipato
cha chini ndilo hitaji lao kubwa,” alisema.
Alisema sababu nyingine
ni kutokana na utawala bora uliopo ndani ya
CCM pamoja na kuwepo viongozi wenye uchu wa kuwaletea wananchi maendeleo.
Hamisi alidai kuwa, viongozi wa CHADEMA hawapo kwa ajili ya
kuwatumikia Watanzania, bali wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Alisema hakulazimishwa wala kufuatwa na viongozi wa CCM ili kumshinikiza
ajitoe CHADEMA, bali alifanya hivyo kwa mapenzi yake na kuwataka viongozi wa
upinzani, kuachana na siasa za propaganda za kudai CCM imekuwa ikiwafuata viongozi wao na kuwahujumu.
Mara baada ya kuwapokea wanachama hao, Kanali mstaafu Lubinga,
alisema CCM ni chama kinachojitambua na kushughulikia matakwa ya wananchi wake
kwa vitendo, bila kujali hali ya kipato chao.
Kanali Lubinga alisema katika kudhihirisha hilo, serikali ya
awamu ya tano imeanza kuwashughulikia mafisadi walioko katika serikali na kwamba,
wapo baadhi ya mafisadi walioko katika Chama na kuwataka wajiandae kwani hawapo
salama.
Aliwataka wananchi wa jimbo la Hai, wanapokwenda katika nyumba
za ibada kusali, wakumbuke kumuombea mbunge wao ili aweze kurudi na kusikiliza
kero zao na kuzifutia ufumbuzi, badala ya kukaa Dar es Salaam muda wote na kula
bata.
LAIZER: CHADEMA INAANDIKA TAARIFA ZA UONGO
ALIYEKUWA Diwani wa Kata ya Ngabobo (CHADEMA), wilayani Meru
mkoani hapa, Solomon Laizer, amekitaka chama hicho kuacha kuandika taarifa za
uongo kwenye mitandao ya kijamii dhidi yake.
Laizer, alijiuzulu nafasi hiyo wiki iliyopita na kuhamia Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na gazeti
hili jana, Laizer alisema taarifa iliyotolewa na Katibu wa CHADEMA, Kanda ya
Kaskazini, Aman Golugwa, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari na baadaye
kurushwa katika mitandao ya kijamii, kwamba
barua yake ya kujiuzulu hakuandika yeye wala kutia saini, ni za uongo na
kuwataka wananchi wazipuuze.
Kwa mujibu wa Laizer, aliandika barua hiyo akiwa na akili timamu , nyumbani
kwake Ngabobo na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Chirstopher Kazeri, Julai 9, mwaka huu.
"Taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya katibu
wa CHADEMA kanda ya Kaskazini dhidi yangu sio za kweli, sijafanya kikao na
CHADEMA na barua yangu ya kujiuzulu nimeandika pekee yangu na kutia saini yangu,
kisha kuiwasilisha kwa mkurugenzi wa Meru kwa mkono wangu mwenyewe,"alisema.
Laizer alisema alifanya maamuzi ya kuondoka CHADEMA na kujiunga
na CCM kwa utashi wake, baada ya kuona kazi nzuri inayoyofanywa na Rais Dk.John
Magufuli.
"Nilitafakari nikaona nchi ilikuwa inahitaji Rais
mzalendo na Mungu ametupa Rais Magufuli, ambaye amejitoa mhanga kutetea
rasilimali za nchi zilizokuwa zinawanufaisha watu wachache pamoja na kutatua
kero mbalimbali za wananchi wanyonge. Haya yote tulikuwa tunayahitaji kwa nini
nisimuunge mkono?” Alihoji.
Alisema aliamua kuachana na CHADEMA na kurudi CCM ili aweze
kumuunga mkono Rais Magufuli kwa utendaji wake uliotukuka hasa wa
kuwashughulikia mafisadi, ambao walikuwa wanatumia rasilimali za nchi vibaya.
"Ninampenda Rais wangu Magufuli, nimeamua kurudi CCM,
sioni sababu ya kuendelea kubaki CHADEMA. Ili niweze kuunga mkono na kumuombea
aendelee kututumikia sisi wananchi wanyonge, nimeamua kurejea CCM,"alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Kazeri alikiri kupokea barua ya Lazeir, Julai 9,
mwaka huu na kwamba, ameshaindikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
No comments:
Post a Comment