Monday, 17 July 2017

WAPIGA DILI DAR WAHAHA


WASIWASI umetanda miongoni mwa watu waliokuwa wakiendesha mambo yao kwa misingi ya kupiga dili, kutokana na serikali kuanza kuchukua hatua dhidi yao.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni umebaini kuwa, baadhi ya watu hao kwa sasa wanahaha kujaribu kukwepa mkono wa sheria, ikiwemo kubadilisha majina ya kampuni zao, kuhama Dar es Salaam na kukimbilia mikoani na nje ya nchi.

Mbali na hilo, imebainika kuwa baadhi ya watu waliokuwa wakijipatia fedha na kujilimbikizia mali, wameanza kutafuta namna ya ama kuziuza au kubadili miliki zake.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili umebainia kuwa, wapiga dili wanaohaha usiku na mchana ni wale waliokuwa na mtandao wa kusafirisha au kuzibadili fedha za kigeni kwa kuhusisha maduka ya kubadilishia fedha hizo, yaani Bureau de Change.

Imebainika kuwa, baadhi ya wamiliki wa maduka hayo walikuwa wakitumiwa na wafanyabiashara wakubwa wasio waaminifu, kusafirisha fedha nje ya nchi bila kufuata taratibu.

Mbali na hilo, wamiliki hao walikuwa wakifanya hivyo huku wakishiriki katika ukwepaji wa kodi za serikali kwa muda mrefu.

Mtandao mwingine wa wapiga dili, ambao kwa sasa unahaha ni ule uliokuwa ukijihusisha kudhulumu nyumba na viwanja vya Wakfu kwa kushirikiana na maofisa wa serikali wasio waaminifu.

Uchunguzi huo umezidi kubaini kuwa, mtandao huo ulikuwa ukihusisha wafanyakazi wasio waaminifu wa taasisi za kisheria na wale wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambako walifanikisha kudhulumu nyumba na viwanja katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

"Sasa hivi jamaa wanahaha kutaka kuuza nyumba na wengine kwenda kuishi mikoani au nje ya nchi, maana wanaogopa mkono wa serikali kwa kuwa ni mrefu,"moja ya chanzo chetu cha habari kilithibitisha.

Pia, imeelezwa kuwa, mtandao mwingine wa wapiga dili unaohaha ni ule wa wafanyabiashara, maofisa wa ardhi na watoa huduma za kisheria, ambao walikuwa wakiandika mikataba ya nyumba chini ya kiwango halisi cha bei ili kukwepa kodi.

Imebainika kuwa, baadhi ya watu hao walikuwa wakifanya hivyo ili kujinufaisha binafsi kwa kutaka kujipatia fedha nyingi huku wakiandika mikataba ya uongo ili kudanganya mamlaka za serikali zinazohusika na utozaji wa kodi.

"Usidanganywe na mtu, hapa Dar es Salaam, nyumba nyingi zimeandikiwa mikataba chini ya viwango halisi. Nyumba inauzwa shilingi milioni 700, kwenye mikataba wanakuandikia shilingi milioni 100. Wengi wa wahusika hawa wana mikataba miwili, yaani ule wa kweli na mwingine wa kupeleka kwenye mamlaka za serikali," kilisema chanzo chetu kingine. 

Kiliongeza: "Hawa jamaa wanatafutana maana kwa sasa hakuna mambo ya kuwa na mtu wa kukulinda, kama umekiuka taratibu na kuvunja sheria."

Kwa sasa, serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu na kuwachukulia hatua stahiki watu waliokuwa wakijihusisha na ukwepaji wa kodi, utakatishaji wa fedha na matukio mengine yaliyo kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment