Monday 17 July 2017

MAJALIWA: MITUMBA SASA BASI



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akionyeshwa ubora wa kanga zinazotengenezwa hapa nchini, katika Kiwanda cha NIDA, alipofanya ziara kwenye kiwanda hicho, Dar es Salaam, jana. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Muhammadhamza Rafiki na kushoto ni Meneja Mkuu, Muhammad  Waseem. (Picha Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwepo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.

Pia, amesema uwepo wa viwanda hivyo utasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika, hivyo aliwataka walime pamba ya kutosha ili viwanda vipate malighafi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi, alipotembelea Kiwanda cha Nyuzi cha Namera, kilichoko Gongo la Mboto na Kiwanda cha NIDA, kilichoko Ubungo, Dar es Salaam.

Alisema viwanda vya kutengeneza nguo nchini ni ushahidi tosha kwamba, nchi iko njiani kuondokana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa zinatengenezwa nchini, hivyo kupatikana kwa bei nafuu.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwa sasa wanunuzi wa pamba hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi, badala yake wauze katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha zitakazouzwa nchini kwa gharama nafuu.

“Pamba yote inaweza kuchakatwa nchini, hivyo hakuna haja ya kuiuza nje ya nchi. Natoa wito kwa wakulima wa pamba, walime vya kutosha kwa sababu soko la uhakika lipo na hii ndio safari ya mwisho ya mitumba,” alisisitiza Majaliwa.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea Kiwanda cha Saruji cha Lake, kinachozalisha saruji ya nyati, ambapo aliwapongeza wawekezaji nchini kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.

Kiwanda hicho, ambacho kinazalisha tani 700,000 kwa mwaka, kimeajiri watu 2,000 na kinalipa kodi  sh. bilioni 81.312 kwa mwaka. Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka watumishi wake wawe waaminifu, wafanye kazi kwa weledi na wawe waadilifu.

Pia, alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vyote nchini, kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi waishio katika maeneo ya karibu na viwanda sambamba na kulipa kodi kwa wakati na kwa viwango sahihi.

No comments:

Post a Comment