Wednesday 12 July 2017

'HAPA KAZI TU' YA RAIS MAGUFULI YAWANG'OA VIGOGO CHADEMA



MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa FFU ulioko Kata ya Terati, mkoani hapa, Anachritus Edward (CHADEMA), amejiuzulu wadhifa wake na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, chama hicho wilayani Arumeru, kimeendelea kusambaratika baada ya Diwani wa Kata ya Ngobobo, Solomon Laizer, kujiuzulu wadhifa wake.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, mjini hapa jana, Edward alisema amechoshwa na siasa za CHADEMA na urasimu uliopo na kwamba, ameamua kurudi CCM kutokana na utendaji kazi mzuri wa Rais Dk. John Magufuli.

"Nimeamua kurudi CCM kwa sababu siridhishwi na mwenendo wa kilichokuwa chama changu cha CHADEMA. Kunapokuwa na migogoro ndani ya chama, tukipeleka malalamiko katika ngazi za juu kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi, hatusikilizwi," alisema.

Edward alisema ameamua kurudi CCM kwa sababu ni Chama kinachowasikiliza wananchi wanyonge pamoja na kutatua kero zao.

Alisema Rais Magufuli amefanyakazi kubwa ya kutetea maslahi ya nchi pamoja na kutatua kero za wananchi wanyonge, ambao walikuwa na kero mbalimbali zinazowakabili kwa muda mrefu.

"Nampongeza Rais wangu Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Dhamira yangu inanisuta kuendelea kubaki CHADEMA, kutokana na urasimu uliopo wa kutosikiliza kero za viongozi wao wa chini," alisema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa mtaa wa FFU,
walimpongeza mwenyekiti huyo kwa kurudi CCM, ambayo walisema imetatua kero mbalimbali za wananchi, hasa wa kata ya Murieti, ambayo ni mpya.

Edward, amekuwa kiongozi wa pili wa upinzani kujitoa katika chama hicho na kujiunga na CCM. Hivi karibuni, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Terati, Kifukwe,
alijivua nafasi yake ya udiwani kutokana na kukunwa na sera na utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambayo alisema inatekelezwa kwa vitendo.

Wakati huo huo, kujiuzulu kwa diwani wa Arumeru, kumefikisha idadi ya madiwani wa kata waliojizulu kwa kipindi cha wiki tatu kufikia watatu na mmoja wa viti  maalumu.

Madiwani hao ni wa Kata ya Makiba, Immanuel Mollel, Anderson Sirikwa  na Josephine Mshiu wa Viti Maalumu.

Akizungumza baada ya kukabidhi barua yake kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Christopher Kazeri, kuhusu kujiuzulu wadhifa ho, Laizer alisema amekunwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

"Nilikuwa diwani wa kata ya Ngabobo kupitia CHADEMA, lakini baada ya kuona Rais Magufuli anafanyakazi nzuri ya kurejesha heshima ya nchi na kutetea wananchi, hasa sisi wanyonge, nimeona ni vyema nikarudi CCM kutokana na sera zake, ambazo zinatekelezwa kwa vitendo," alisema diwani huyo.

Alisema kuondoka CHADEMA hakutamuathiri kwa kuwa wananchi wa kata yake waliomchagua, wameunga mkono kuondoka kwake CHADEMA na kwamba, wapo nyuma yake kurudi CCM.

Alisema Rais Dk. Magufuli ni zawadi kwa wananchi wa Tanzania waliyopewa na Mungu na kuwaomba kuendelea kumuombea ili aweze kuwatumikia na kulinda rasilimali za nchi.

No comments:

Post a Comment