Tuesday, 18 July 2017
JPM KUFANYA ZIARA MIKOA MINNE, KUZINDUA MIRADI TISA
RAIS Dk. John Magufuli, anatarajiwa kufungua na kuzindua miradi tisa ya barabara na uwanja wa ndege katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Singida, kuanzia kesho hadi Jumanne ijayo.
Taarifa iliyotolewa jana na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, ilisema kesho atafungua barabara ya Kigoma- Biharamulo – Lusahunga, yenye urefu wa kilomita 154, ambapo ufunguzi huo utafanyika Biharamulo, mkoani Kagera.
Alisema Julai 21, mwaka huu, atazindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Nyakanazi - Kibondo, yenye urefu wa kilomita 50, ambao utafanyika Kakonko mkoani Kigoma.
Pia, Rais Dk. Magufuli siku hiyo atazindua ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kidahwe- Kasulu, yenye urefu wa kilomita 63, utakaofanyika mkoani Kigoma.
Julai 23, mwaka huu, Rais Magufuli atafungua barabara ya Kaliua – Kazilambwe, yenye urefu wa kilomita 56, ambao utafanyika Kaliua mkoani Tabora.
Mhandisi Mnyamhanga aliongeza kuwa, siku hiyo kutafanyika ufunguzi wa barabara ya Urambo-Ndono-Tabora, yenye urefu wa kilomita 56, utakaofanyika Urambo Mjini.
Alisema Julai 24, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli atafungua barabara ya Tabora-Puge-Nzega, yenye urefu wa kilomita 114.9, ambao utafanyika Tabora Mjini.
Katibu Mkuu huyo alisema siku hiyo hiyo, atafungua barabara ya Tabora - Nyahua, yenye urefu wa kilomita 85.
Pia, atafungua uwanja wa ndege wa Tabora na barabara ya Manyoni-Itigi- Chaya, yenye urefu wa kilomita 89.3 na ufunguzi wake utafanyika Itigi mkoani Singida.
Alisema kukamilika kwa ujenzi kwa kiwango cha lami wa miradi ya barabara na kuzinduliwa kwa miradi mipya ya ujenzi wa barabara katika ukanda wa kati na ukanda wa magharibi, ni sehemu ya utekekelezaji wa azma ya serikali ya kuunganisha makao makuu ya mikoa yote nchini na nchi jirani kwa barabara za lami.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment