Tuesday, 18 July 2017

MWILI WA MKE WA DK. MWAKYEMBE KUAGWA LEO


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, leo anatarajia kuwaongoza Watanzania katika kuuaga mwili aliyekuwa mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana, msemaji wa familia, Salomoni Kivuyo,  alisema kutakuwa na ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKT) Usharika wa Kunduchi.

Msemaji huyo alisema mwili wa marehemu Linah Mwakyembe, unatarajiwa kuwasili nyumbani kwake Kunduchi, saa tatu asubuhi na shughuli ya kuuga na ibada zitafanyika baada ya muda huo nyumbani hapo.

"Baada ya kuwasili, mwili utapelekwa kanisani na kufanyika ibada na baadaye kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, saa saba mchana, ambako utasafirishwa kwenda Mbeya kwa maziko,"alisema.

Wakati huo huo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, aliyekuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Paul Makonda, jana walikwenda nyumba kwa Dk. Mwakyembe kumpa pole.

George Mwakyembe, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Dk. Mwakyembe, alisema kifo cha mama yake ni pigo kubwa kwa familia kutokana na mchango wake.

Alisema mama yao alikuwa akiwafundisha misingi ya maisha na misimamo bora huku akitekeleza majukumu yote kama mama wa familia.

Kwa upande wake, Jaji Lubuva alisema Linah alikuwa mchapakazi, hivyo ni pigo kubwa kwa familia na serikali kutokana na utendaji wake.

Alisema katika msiba huo, amejifunza kitu ambacho wanafamilia wa Mwakyembe wamekuwa wakikifanya katika jamii, hivyo ni jambo zuri la kuiga mema aliyoyafanya.

Linah, alifariki Julai 16, mwaka huu, katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya saratani ya matiti.

No comments:

Post a Comment