Tuesday 18 July 2017

SHIBUDA: ACHENI WIVU NA HUSUDA KWA RAIS MAGUFULI


VYAMA vya upinzani nchini vimetakiwa kuacha wivu na husuda, badala yake vipongeze juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, katika kupigania rasilimali za Watanzania.

Wito huo ulitolewa jana, mjini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda, alipokuwa akizungumza na Uhuru.

Shibuda alisema vyama vya siasa vinatakiwa kufahamu kuwa, vina wajibu wa kufanya siasa za uzalendo na uaminifu kwa maslahi ya jamii na uchumi wa taifa.

“Wanasiasa tuwekeni kando tofauti na mitazamo ya makundi binafsi ya kujenga umaarufu wa umimi na usisi, usioboresha suluhu za ushindi kwa maslahi ya taifa,” alisema.

Vilevile, aliwaasa wanasiasa, wanataaluma na wananchi kwa ujumla wao, kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli, ambaye anapigania haki na usawa wa rasilimali za Watanzania.

“Wanasiasa, wafurukutwa na wanaharakati wapenda siasa wote, tuna wajibu wa kutambua na kukiri kwamba, kipaumbele cha chama chochote ni siasa zenye maslahi ya wanachama wazalendo, watiifu na waaminifu kwa usalama wa uhuru wa taifa hili. Hivyo tumuunge mkono Rais Magufuli,” alisema.

Pia, aliwataka Watanzania kutoa mawazo na ujuzi wao katika kupigana vita ya uchumi, ambayo inaendelea nchini.

“Natoa wito kwa kila Mtanzania, afikirie mbinu za kuwa hodari kwa nguvu za hoja za kudai haki na usawa kwa maliasili za ardhi yetu. Tuache kauli za uchoyo dhidi ya vita hii ya uchumi,” alisema.

Alisema Watanzania wapo katika vita ya kujikomboa na kuithibitishia dunia kuhusu uhai wa umoja wa utaifa wa wanasiasa katika kulinda na kuendeleza ndoto za madai ya uhuru wa jamii na taifa.

“Tuiambie dunia iwe na imani ya kuwa tunaweza kujiongoza na tunaweza kujitawala na kujitegemea. Kwa hiyo sote tulinde uhuru na usalama wa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania,” alisema.

Pia, alivitaka vyama vya upinzani kuweka tofauti zao pembeni na kuungana na Rais Magufuli katika vita ya kudai haki na usawa na kuachana na kasoro zote zilizowahi kutokea kipindi cha nyuma.

Vilevile, alivitaka vyama hivyo kuacha kushabikia kasoro zilizowahi kuwa mirefeji iliyotumika kutoroshea maliasili za nchi, badala yake waungane na Rais Magufuli kupigania rasilimali za nchi.

“Tumuunge mkono Rais wetu, tumuunge mkono hata kimawazo, tumpe umoja wa fikra ili aweze kusonga mbele,” alisema.

No comments:

Post a Comment