Tuesday, 18 July 2017

LOWASSA AMECHUJA- DK. BANA


WAZIRI Mkuu aliyestaafu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ameonekana hana mvuto kwa Watanzania, kutokana na kasi anayoenda nayo Rais Dk. John Magufuli, kwa kuwasaidia wanyonge na kuleta uzalendo.

Baadhi ya wadau wa siasa nchini wamesema, Lowassa ni haki yake  kugombea tena urais mwaka 2020, kwa mujibu wa Katiba ya nchi inavyosema, lakini anatakiwa atafakari kwa kina ndipo aanze kujitangaza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema hayo jana na kuwataka viongozi wa kisiasa, wasiweke tamaa ya madaraka mbele bila ya kujua watawafanyia nini Watanzania wa leo na hata vizazi vijavyo.

"Kila kitu kinakwenda na wakati wake. Hivi sasa, Lowassa hana mvuto kwa Watanzania, amepoteza sifa ile aliyokuwa nayo awali. Kama ni ua, basi ni lile ambalo limekosa maji na mbolea, hivyo haliwezi kun'gara na kupendwa na watu kama ilivyokuwa zamani," alisema Dk. Bana.

Hata hivyo, msomi huyo alisema ni mapema mno kwa Lowassa kutangaza kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Dk. Bana alisema anachotakiwa kufanya Lowassa hivi sasa sio kujitangaza kuwa atagombea urais, bali atafute taasisi yoyote ili iweze kumfanyia utafiti ajue ni Watanzania wangapi, ambao bado wanamkubali.

Pia, alisema kasi anayoenda nayo Rais Dk. Magufuli ni kizuizi kikubwa kwa Lowassa na wagombea wengine watakaojitokeza kushinda uchaguzi huo.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholaus Mgaya, alimtaka Lowassa kufuata nyayo anazokanyaga Dk. Magufuli.

"Ukweli ni kwamba, Rais Magufuli ametufanya Watanzania kuwa pamoja na amerudisha uzalendo uliokuwepo hapo awali," alisema Mgaya.

Alisema kwa kasi anayokwenda nayo Dk. Magufuli, ni vigumu kwa Lowassa kushinda urais.

Kwa upande wake, mwanaharakati Shiganga George alisema: "Rais Dk. Magufuli anafuata sera za CCM na anatimiza ahadi zake kwa Watanzania kwa kile alichowaahidi kipindi cha kuomba kura mwaka 2015."

George alisema Watanzania wanapenda kuona mageuzi hata kwa viongozi wengine, lakini viongozi wenyewe wanaonyesha uchovu pale wanapokwenda kuwawakilisha wananchi bungeni.

Hivi karibuni, Lowassa amekuwa akitakiwa kuripoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, kutokana na kauli yake kuhusu viongozi wa Jumuia ya Uamsho, waliokamatwa mwaka 2012 huko Zanzibar.

No comments:

Post a Comment