Tuesday, 18 July 2017
NEMC YAFUMULIWA, BAADHI YA VIGOGO WATUMBULIWA, WENGINE WAHAMISHWA
SERIKALI imelifumua Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kutokana na tuhuma za vitendo vya rushwa na urasimu katika mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira.
Hatua hiyo ilichukuliwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, ambapo vigogo wanne wamesimamishwa kazi huku uteuzi wa wajumbe saba wa bodi ya baraza hilo ukitenguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Makamba alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Kifungu cha 19 (2), ametengua uteuzi wa wajumbe hao huku watumishi wengine wakipangiwa vituo vipya vya kazi.
Waziri Makamba aliwataja waliosimamishwa kazi kuwa ni Mwanasheria Mkuu wa NEMC, Manchare Heche, Deus Katware, Andrew Karuwa na Benjamini Doto na kwamba, wengine watafuata baada ya uchunguzi kukamilika.
Mbali na hilo, Makamba amemteua Dk. Elikana Kalumanga kutoka Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili ya Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM), kuwa Kaimu Mkurugenzi wa baraza hilo hadi hapo Rais Dk. John Magufuli atakapofanya uteuzi.
"NEMC ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa mazingira na mustakabali wa maendeleo endelevu katika sera ya viwanda, hivyo utendaji wake umekuwa ukilegalega na umekuwa hauridhishi,"alisema.
Aliongeza kuwa, kutokana na hatua hiyo ya ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa Tathmnini ya Athari kwa Mazingira (EIA) na tuhuma za rushwa, kuna haja ya kuifumua na kuisuka upya NEMC.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni watumishi kutokuwa na lugha nzuri kwa wateja na kuwatisha ili watoe chochote na kutumia kampuni binafsi ya watumishi wa NEMC kufanya kazi za ukaguzi.
"Kumekuwa na tabia ya kuwaelekeza wawekezaji kwenda kwenye kampuni kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari kwa mazingira, ambayo yanamilikiwa au yenye ubia na watumishi wa NEMC, bila kujali mgongano wa kimaslahi, mambo ambayo hayaruhusiwi,"alifafanua.
Alisema kwa kipindi kirefu serikali imejitahidi kufanya marekebisho yanayotokana na hali hiyo, lakini bado haikufanikiwa, hivyo imebainika kuwa matatizo hayo yanatokana na usimamizi usio imara wa bodi na watendaji wakuu.
"Tumefanya mabadiliko makubwa ili kuboresha hali ya utendaji, ambapo wakurugenzi na wakuu wa kanda wamepangiwa vituo vipya,"alisema
Alimtaja Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa NEMC, Charles Wangwe kuwa amerejeshwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine na kwamba, nafasi hiyo itachukuliwa na Adam Minja kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Wengine ni Risper Koyi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, ambaye ameteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria NEMC, kuchukua nafasi ya Wanjara Jandwa, ambaye anahamishiwa Kanda ya Kati - Dodoma.
"Tumemteua Dk. Yohana Mtoni, Ofisa Mazingira Mkuu wa NEMC kuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Sheria, kuchukua nafasi ya Dk. Ruth Rugwisha, ambaye anakuwa Mkuu wa Kanda ya Ziwa -Mwanza. Pia, tumemteua Carlos Mbuta, aliyekuwa Ofisa Mawasiliano Mkuu wa NEMC kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa NEMC,"alifafanua.
Makamba aliwataja baadhi ya wakuu wa kanda, ambao wamepangiwa vituo vipya kuwa ni Jafari Chimgege, aliyekuwa Mkuu wa Kanda ya Mashariki, ambaye amehamishiwa Kanda ya Kati.
Goodlove Mwamsojo, aliyekuwa Kanda ya Mashariki - Dar es Saalam,
anakwenda Kanda ya Nyanda za Juu; Dk. Vedastus Makota, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma atahamishiwa Kanda ya Kusini - Mtwara.
Waziri Makamba aliongeza kuwa, baada ya mabadiliko hayo, miradi yote ambayo itapelekwa NEMC, ya kuomba kupata cheti cha EIA, ni ile ambayo tayari imefanyiwa kazi na washauri elekezi.
Aliagiza NEMC kufuta orodha ya watu binafsi na kampuni zote za ushauri wa EIA, ambazo hazina sifa au zimeshindwa kutekeleza kazi zao vizuri.
Pia, aliagiza baraza hilo liweke bei elekezi na ukomo kwa waelekezaji hao kila aina ya miradi inayotakiwa kufanyiwa EIA na kwamba, hakuna mshauri mwelekezi, ambaye ataenda juu ya bei elekezi katika kundi la miradi husika.
"Tunaamini mabadiliko haya yatatoa mwanzo mpya katika utendaji wa NEMC, hasa katika kusimamia uzingatiaji wa sheria ya mazingira, pia uharakishaji wa miradi ya maendeleo na uwekezaji nchini, hasa ujenzi wa viwanda ili kutekeleza azma ya Rais Dk. Magufuli,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment