Thursday 20 July 2017

MAJALIWA AWAONYA WANAOITUKANA, KUIKEJELI SERIKALI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwakemea viongozi wa kisiasa wanaotoa matamko ya matusi na kejeli dhidi ya serikali.

Pia, amesema serikali ya awamu ya tano itaendelea kuwachukulia hatua viongozi wa kisiasa watakaokuwa chanzo cha mfarakano kwa jamii kutokana na matamko yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana, katika kijiji cha Ikolo, Kyela, wakati wa mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Linah.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Samuel Malicela na mkewe, Anne Kilango na baadhi ya wabunge, akiwemo Joseph Mbilinyi wa Mbeya Mjini.

Majaliwa alisema serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayehatarisha amani ya nchi, iwe kwa wadhifa wake au cheo chake, kwa kuwa imedhamiria kuwatumikia wananchi.

"Tunashukuru viongozi wa dini kulizungumzia hilo hapa, endeleeni na msikate tamaa kuwakemea wale wote wanaotoa matamko ya hovyo kwa jamii,"alisema.

Kauli ya Waziri Mkuu ilitokana na mahubiri ya Askofu Rabison Mwakanani wa Kanisa la Evangilical Brotherhood Tanzania, aliyeongoza ibada ya kumuombea marehemu, iliyofanyika kwenye makaburi ya familia kijijini hapo.

Askofu Mwakanani alisema, umefika wakati wa wanasiasa kufikiri maneno wanayoyatoa kwa jamii kabla ya kuyatamka ili kulinda amani na mshikamano uliopo.

Alisema Rais Dk. John Magufuli amekuwa akifanyakazi nzuri na kubwa, ambayo kila Mtanzania anapaswa kuipongeza, hivyo anayoyafanya sio ya kubezwa.

"Waziri Mkuu, mimi sina jukwaa la kisiasa, lakini nashukuru hapa kwenye msiba nimepata jukwaa la kuzungumza na kuwakemea wote wanaotoa maneno ya kashfa dhidi ya viongozi,"alisema.

Alisema hivi karibuni, alipita kwenye kijiwe kimoja cha vijana eneo la Soweto, mjini Mbeya na kuwakuta wakibishana maneno ya wanasiasa, ambayo dhahiri ni uchochezi mtupu.

Hivyo, alisema ni wakati wa wanasiasa na viongozi kutafakari kabla ya kuzungumza mambo kwa kuwa ni muhimu kulinda amani ya nchi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa akimzungumzia marehemu Linah, alisema alikuwa mtu mwenye upendo na anamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema.

Alisema anajua fika Waziri Dk. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu kutokana na msiba huo, lakini anaamini serikali ipo pamoja naye katika wakati huu mgumu.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimpa pole Waziri Dk. Mwakyembe huku akiitaka familia kuendelea kuwa na upendo kama ule uliokuwepo, ambao waombolezaji wengi katika msiba huo waliuelezea.

Kwa upande wake, mtoto mkubwa wa marehemu, Gabriel, alisema anaamini mama yao alijiandaa na kifo hicho kwa kuwa alikuwa mcha Mungu.

"Mama alikuwa na ratiba kila siku ifikapo saa nne usiku, lazima afanye ibada. Hivyo nina matumaini makubwa kupitia ucha Mungu wake kwamba, Mwenyezi Mungu atamweka mahala pema," alisema

Kwa upande wake, Waziri Dk. Mwakyembe aliwashukuru viongozi wote wa kiserikali, akiwemo Rais Dk. Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Majaliwa, kwa kuwa mstari mbele katika kumuuguza mkewe hadi anafariki.

Alisema mkewe amekufa kwa saratani ya titi, ambapo alidai alipanga endapo akipona, atawapigania wanawake wenzake kupambana na ugonjwa huo.

Dk. Mwakyemba alisema, ndoto ya mkewe haijatimia, lakini anaamini ataitekeleza katika siku zijazo ili kuunga mkono jitihada aliyokuwa nayo.

No comments:

Post a Comment