Thursday, 20 July 2017

MANJI ANASA GEREZA LA KEKO



MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ameshindwa kufika mahakamani akitokea mahabusu Gereza la Keko, kutokana na kuwa mgonjwa.

Kwa sasa, mfanyabiashara huyo yuko katika hospitali ya Gereza la Keko kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, alidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati shauri hilo linalomkabili Manji na wenzake watatu, lilipopelekwa kwa kutajwa.

Katuga alidai Manji, ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ya jinai, hayupo mahakamani hapo, ambapo kwa mujibu wa taarifa za daktari, anaumwa na yuko hospitali ya Gereza la Keko anatibiwa.

Wakili huyo alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa wataendelea kubaki rumande.

Mbali na Manji (41), washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Meneja Rasilimali Watu, Deogratius Kisinda (28), mtunza stoo Abdallah Sangey (46) na mtunza stoo msaidizi, Thobias Fwele (43) mkazi wa Chanika.

Mfanyabiashara huyo na wenzake, wanakabiliwa na mashitaka saba, yakiwemo ya kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mihuri ya JWTZ.

Mashitaka hayo yanayowakabili, yanaangukia chini ya Sheria za Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa, ambapo siku ya kwanza waliposomewa mashitaka hayo, Julai 5, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) aliwasilisha hati ya kupinga wasipewe dhamana.

Washitakiwa hao walisomewa mashitaka hayo wakiwa katika wodi namba moja ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, iliyoko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya mahakama kuamua kuhamia hospitalini hapo kwa ajili ya kumsomea mashitaka Manji, aliyekuwa amelazwa.

Kutokana na hali hiyo, washitakiwa wenzake watatu nao ilibidi wapelekwe hospitalini hapo, wakitokea kituo cha polisi ili waweze kusomewa mashitaka pamoja.

Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na DPP hajawasilisha hati ya kuipa mamlaka ya kusikiliza.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kupinga dhamana ya DPP, ambapo ilipingwa na mawakili wa washitakiwa hao, hivyo kuifanya mahakama itoe uamuzi kwamba, haiwezi kuzungumza lolote kuhusu hilo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Manji na wenzake wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe ‘A’, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na ofisa wa polisi wakiwa na mabando 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za jeshi hilo, zenye thamani ya sh. milioni 192.5, ambavyo vilipatikana isivyo halali.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa Julai mosi, mwaka huu, katika maeneo hayo, walikutwa na ofisa wa polisi, wakiwa na mabando manane ya vitambaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 44.

Shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na mhuri wa JWTZ, wenye maandishi “MKUU WA KIKOSI 121 KIKOSI CHA JESHI JWTZ”,  bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo, walikutwa na mhuri wa JWTZ, wenye maneno “KAMANDA KIKOSI 834 KJ MAKUTUPORA DODOMA,” bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Manji na wenzake, pia wanadaiwa siku hiyo walikutwa na mhuri mwingine wenye maneno 'COMANDING OFFICER 835 KJ, MGAMBO P.O BOX 224 KOROGWE'.

Washitakiwa hao wanadaiwa Julai mosi, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na vibao vya namba za usajili za magari vyenye namba SU 383 na SM 8573, ambavyo vilipatikana isivyo halali.

No comments:

Post a Comment