Monday, 24 July 2017
MARUFUKU KUVUTA SIGARA HADHARANI ZANZIBAR
WIZARA ya Afya Zanzibar, imepiga marufuku matumizi ya sigara katika maeneo ya wazi na sehemu za kutolea huduma za umma.
Imesema imefikia uamuzi huo kwa lengo la kupambamba na matumizi ya sigara ili kulinda afya za wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba, Bakar Ali Bakar, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja juu ya kanuni ya kudhibiti matumizi ya sigara na tumbaku, yaliyofanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Michezo wa Gombani, Chake Chake, Pemba.
Aliyataja maeneo ambayo ni marufuku kwa mtumiaji wa sigara kuyatumia kuwa ni masoko, majengo ya burudani, vituo vya afya, skuli na maeneo mengine yenye mkusanyiko wa watu.
"Kuanzia leo ni marufuku matumizi ya sigara kwenye sehemu za wazi, ambazo zina mkusanyiko wa watu. Kama mtu anataka kuvuta sigara, anapaswa kutafuta sehemu, ambayo moshi wa sigara hauwawathiri walio karibu,"alisema.
Ofisa huyo pia alisema sheria hiyo inazuia mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18, kuuza au kutoa matangazo ya biashara ya tumbaku, sambamba na vyombo vya habari kutangaza au kudhamini matangazo hayo.
Alisema serikali kupitia wizara hiyo, haitakuwa tayari kuona vitendo vya watoto walio chini ya umri wa miaka 18, wakihusika katika matangazo hayo na kuwataka waandishi wa habari kusaidia kuufikisha ujumbe huo wa wananchi .
Akiwasilisha vifungu vya kanuni ya kudhibiti matumizi ya tumbaku Zanzibar, Mratibu wa Kitengo cha Maradhi yasiyoambukizika, Dk. Omar Mwalim Omar, aliwataka waandishi wa habari kusaidia kuitangaza kanuni hiyo ili kudhibiti matumizi ya tumbaku nchini.
Katika mafunzo hayo yaliwashirikisha waandishi wa habari, maofisa wa polisi, wakuu wa mabaraza ya miji, halmashauri na Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment