Tuesday, 25 July 2017

MABILIONEA 26 KUTOKA YPO WATUA NCHINI, WATEMBELEA HIFADHI YA SERENGETI

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, akizungumza na mabilionea hao jana, katika moja ya hoteli ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Alan Kijazi.

KIONGOZI wa msafara wa mabilionea hao, Perry Amber, akizungumza wakati wa mapokezi hayo.

MABILIONEA hao wakimsikiliza Waziri Maghembe.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amewakaribisha nchini wafanyabiashara mabionea 26, kutoka Taasisi ya Young Presidents Organization (YPO).

Mabilionea hao kutoka mabara yote duniani, waliwasili nchini juzi na kupokewa na Profesa Maghembe, kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo jana, ilisema kuwa mabilionea hao wamekuja nchini kwa ziara ya siku tatu ya kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii.

Ujio wa mabilionea hao ni sehemu ya ziara yao katika nchi nane duniani, zikiwemo Uingereza, Rwanda, Maldives, Nepal, Bhutan na Rajastan.

Katika hafla ya chakula cha jioni, aliyowaandalia wageni hao juzi, Profesa Maghembe, aliwakaribisha nchini ili kujionea maajabu ya dunia yanayobebwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Hakuna eneo lolote katika uso wa dunia lenye mkusanyiko wa wanyama wanaokula majaji (hebrivores) na wale wanaokula nyama (canivores) kama Serengeti,"aliwaambia wageni hao.

Waziri huyo pia aliwaeleza wageni hao kuwa, uhifadhi ni gharama kubwa inayobebwa na Tanzania kwa niaba ya dunia.

Aliwaomba wakawe mabalozi wa kuitangaza Tanzania kama eneo lenye amani na vivutio vyenye ubora wa pekee, hatua itakayoiwezesha kupata watalii wengi zaidi na kuiongezea mapato.

Aidha, aliwaomba wageni hao warudi tena nchini kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda ili kukuza uchumi wa nchi, unaokua kwa wastani wa asilimia saba kwa kipindi cha miaka 15.

Ziara ya mabilionea hao imekuja siku chache baada ya ujio wa timu ya Everton ya England, ambayo ilicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo, Everton ilishinda mabao 2-1.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, Tanzania imekuwa kivutio kikubwa cha utalii duniani, ambapo katika muda wa miezi miwili iliyopita, imepokea wasanii na wanamichezo mbalimbali maarufu duniani.

Hivi karibuni, mwanamuziki nyota wa Marekani, Usher Raymond, alitua nchini akiwa na familia yake na kutembelea Mbuga ya Serengeti.

Wasanii na wanamichezo wengine nyota duniani, waliotembea nchini hivi karibuni ni David Beckham, Morgan Schneiderlin, Mamadou Sakho, Victor Wanyama, Christian Erikssen, Sanjay Dutt na Will Smith.

No comments:

Post a Comment