Tuesday, 25 July 2017

TUNDU LISSU KUSOTA SEGEREA SAA 72



MBUNGE Tundu Lissu (Singida Mashariki-CHADEMA), atasota kwenye mahabusu ya Gereza la Segerea kwa saa 72, kusubiria uamuzi wa kupatiwa dhamana au la kutokana na tuhuma za kutoa lugha ya uchochezi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Lissu, kupandishwa kizimbani jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri, ambako kuliibuka mabishano ya kisheria, baada ya serikali kupinga asipewe dhamana.

Mbunge huyo alifikishwa mahakamani hapo saa 5.50 asubuhi, akitokea mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, alikokuwa akishikiliwa tangu Alhamisi, iliyopita na kunyimwa dhamana ya polisi, hivyo kukaa ndani kwa saa 96.

Lissu (49), ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, baada ya kufikishwa kwa kutumia gari aina ya Land Cruiser, lenye namba T886 BWX, likiwa na vioo vya kiza, alipelekwa kwenye chumba cha mahabusu wanaosubiri kesi zao kuitwa, ambako alikaa kwa saa tatu hadi saa 8.17 mchana, alipopelekwa mahakamani.

Ilipotimu saa 8.24 mchana, Hakimu Mashauri aliingia katika ukumbi wa mahakama namba moja, ambao ulikuwa umefurika watu na Lissu alipanda kizimbani kusomewa shitaka linalomkabili.

SHITAKA LINALOMKABILI LISSU

Jopo la mawakili wa serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa akishirikiana na Mawakili wa Serikali, Wankyo Simon, Paul Kadushi na Tulumanywa Majigo, lilimsomea mshitakiwa shitaka la kutoa lugha ya uchochezi.

Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 17, mwaka huu, maeneo ya Ufipa, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Anadaiwa siku hiyo, alitumia maneno yenye maudhui ya uchochezi yasemayo: “Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini. Vibali vya kazi vimetolewa kwa wamishenari wa kikatoliki tu huku madhehebu mengine yakielezwa kupanga foleni uhamiaji.

"Viongozi wakuu wa serikali wamechaguliwa kutoka kwenye familia, kabila na ukanda. Acheni uwoga, pazeni sauti, kila mmoja wetu tukawaambie wale ambao bado wanampa msaada kwa pesa Magufuli na serikali yake kama tulivyowaambia wakati wa serikali ya makaburu, hii serikali isusiwe na jumuiya ya kimataifa, isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huu wa kibaguzi…yeye ni dikteta uchwara.”

Upande wa jamhuri ulidai  maneno hayo yalikuwa na lengo la kujenga chuki ndani ya jamii.

Baada ya kusomewa mashitaka, Lissu alidai kusema kweli haijawahi kuwa kosa la jinai, hivyo siyo kweli.

Hakimu Mashauri alisema mahakama imeandika mshitakiwa amekana kosa.

Wakili wa Serikali, Wankyo alidai upelelezi bado, lakini kuna hoja kadhaa wanataka kuziwakilisha mahakamani hapo.

SERIKALI YAPINGA LISSU ASIDHAMINIWE

Akiwasilisha hoja hizo, Wakili Wankyo alidai mshitakiwa huyo ana mashauri kadhaa mahakamani, ambayo ni mashauri namba 233/2016, 123/2017, 279/2016 na 208/2016.

Alidai kesi zote zimekuwa zinaashiria au uhalisia wa uchochezi, hivyo ni dhahiri makosa ya namna hiyo yanakuwa yanajirudia, ikijumlishwa na alilosomewa mahakamani hapo.

"Kesi zote zilizoletwa mahakamani dhidi yake zimejikita katika uchochezi na amekuwa akitenda makosa hayo baada ya kutoka mahakamani na kupewa dhamana," alidai.

Alidai ni dhahiri kwamba, kutokana na mwenendo wa mashauri hayo, kumesababisha kutoka katika uchochezi na kwenda kwenye chuki, kama alivyosomewa mahakamani hapo.

“Shitaka alilosomewa leo (jana), limegusa mamlaka mbalimbali za nchi na hata kwa usalama wa nchi, sio jambo la kufumbiwa macho,"alidai.

Wakili huyo alidai kutokana na kujirudia kwa makosa  na kuleta chuki kwa jamii, wanaomba Lissu asipewe dhamana kwa sababu yanaweza kutokea makubwa.

Hoja nyingine iliyowasilishwa na jamhuri ni kuhusu uhalisia wa matamshi yenyewe yaliyosomwa kwenye hati ya mashitaka. Wakili Wankyo alidai matamshi hayo siyo ya kawaida, yanasababisha chuki baina ya Watanzania na madhara yake sio madogo kama yataachwa na kunyamaziwa.

Wankyo  alidai matamshi hayo yamegusa udini, ukabila, familia na ukanda hivyo ni dhahiri  siyo ya kawaida.

"Tunaiomba mahakama kutokana na uzito wa matamshi hayo yaliyotoka kwenye uchochezi kwenda katika chuki, iangalie kwa jicho la ukali na kumnyima dhamana mshitakiwa kwa kuwa anayatoa baada ya kupewa dhamana. Tunaamini hayatajirudia baada ya mshitakiwa  kunyimwa dhamana," alidai.

Kwa upande wake, Wakili Majigo alidai kwa mujibu wa sheria, mahakama hiyo inayo mamlaka ya kumnyima mshitakiwa dhamana kwa ajili ya kutoa ulinzi wake na usalama.

Majigo alidai matamshi yaliyotolewa na mshitakiwa huyo, yanaleta chuki ndani ya jamii, hivyo akirudi uraiani anaweza kupata madhara.

“Tunaomba kwa ajili ya ulinzi na usalama wake, mshitakiwa (Lissu), anyimwe dhamana,” aliomba.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kosa alilolifanya mshitakiwa sio kwamba linagusa tu usalama wake, bali linaenda kubomoa misingi ya umoja, mshikamano na upendo, ambao umejengeka miongoni mwa Watanzania.

“Mahakama inatekeleza majukumu yake kwa sababu kuna amani na umoja unaoongelewa, ndiyo maana hata kifungu anachoshitakiwa nacho cha 63 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na cha 2, kwa kuona uzito wa amani na usalama wa nchi kwa ujumla wake, kimeweka adhabu kubwa,” alidai.

Wakili huyo alidai kifungu hicho kimeweka adhabu ya kutumikia kifungo kisichopungua miaka mitano jela kwa mtu atakayepatikana na hatia.

“Bunge lilitoa adhabu hiyo, kukomesha makosa kama haya. Tunaiomba mahakama ikubali maombi yetu,” waliomba.

MAWAKILI WAMPIGANIA LISSU

Jopo la mawakili takriban 17, lilijitokeza kumtetea Lissu, wakiwemo Fatuma Karume na Peter Kibatala, ambao waliwasilisha hoja zao kupinga mteja wao kunyimwa dhamana.

Wakili Fatuma alikuwa wa kwanza kuwasilisha hoja kwa upande wa jopo hilo, ambapo alidai dhamana ni haki ya msingi ya mshitakiwa na siyo ya serikali wala ya upande wa Jamhuri.

Fatuma alidai Lissu bado hajahukumiwa, hivyo upande wa Jamhuri na serikali unapaswa kukumbuka kuwa, wao ndio waliomshitaki mbunge huyo kwa maneno hayo, ambayo uchunguzi wake haujakamilika.

“Wanataka mahakama imfunge Lissu, kwa sababu tu wao wameamua. Kesi walizotaja dhidi yake zote zimeletwa mahakamani na kuanza baada ya mwaka 2015, kuingia madarakani Rais Magufuli,” alidai.

Wakili huyo alidai kesi hizo zote mpaka ya sasa, hawajakamilisha uchunguzi.

Naye, Wakili Kibatala alidai kosa linalomkabili Lissu sio miongoni mwa makosa ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Pia, alidai hakuna kitu ambacho kimewasilishwa mahakamani hapo na upande wa jamhuri kuthibitisha uwepo wa kesi dhidi ya Lissu mahakamani.

Kibatala alidai ili kumnyima mshitakiwa dhamana, upande wa Jamhuri kwa kushirikiana na polisi, walitakiwa kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo kwa ajili ya kupinga dhamana.

“Hakuna hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani, maneno wanayosema yamekuwa yanaelea hewani,” alidai.

Mbali na hayo, Wakili huyo alidai kwenye hati ya mashitaka, hajaona sehemu ambayo dini imeshambuliwa wala kabila na wala haisemi mahali aliposemea maneno hayo.

Kibatala alidai katika adhabu kuhusu kosa hilo, kuna kifungo au faini.

Kuhusu hoja ya usalama wa Lissu, Kibatala alidai ni jukumu la serikali kumlinda raia wake, hivyo hakuna hoja yoyote ya kisheria, ambayo inaweza kuifanya mahakama imnyime dhamana.

SERIKALI YAWAJIBU MAWAKILI WA LISSU

Wakili wa Serikali, Kadushi alidai hakuna mahali popote, ambapo upande wa Jamhuri unatakiwa kuwasilisha hati ya kiapo kupinga dhamana kwa mshitakiwa.

Kadushi aliiomba mahakama kutazama uhalisia wa matamshi na uzito wa kosa, ikiridhia imnyime dhamana mshitakiwa.

Aidha, alidai wadhifa wa mshitakiwa hauna nafasi yoyote katika sheria, kwa kuwa mshitakiwa  ni raia kama wengine na kama washitakiwa wengine.

Baada ya Kadushi kueleza hayo, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi wiki hii.

LISSU AENDA MAHABUSU

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Lissu aliondolewa katika chumba cha mahakama chini ya ulinzi mkali na hatimaye kuondolewa mahakamani hapo kupelekwa mahabusu.

Msafara wa kumpeleka Lissu mahabusu, ulitoka mahakamani hapo saa 10.31 jioni, ambapo kulikuwa na magari mawili aina ya Land Cruiser ya polisi,
la kwanza lilikuwa limesheheni askari kwa ajili ya kusafisha njia na la pili alikuwepo mshitakiwa huyo.

Katika gari alilokuwepo Lissu, ilikuwa sio rahisi kumuona, kwa kuwa alikuwa amekalishwa chini huku askari waliokuwa wamevalia sare na nguo za kiraia wakiwa wamesimama.

Baada ya kuondoka kwa mshitakiwa huyo, polisi waliokuwepo mahakamani hapo walianza kazi ya kuwaamrisha wanachama wa CHADEMA kuondoka eneo hilo, ambapo walitii amri hiyo.

No comments:

Post a Comment