MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa, ikiwemo kufuatilia kwa karibu vitendo vyenye kuashiria rushwa na utakatishaji fedha.
Amesema juhudi hizo zitaambatana na uimarishaji wa taasisi zinazokabiliana na vitendo hivyo na kutoa elimu kwa wananchi.
Pia, amezitaka taasisi binafsi na vyombo vya habari, kushirikiana na serikali katika kukabiliana na vitendo vya rushwa.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana, Dar es Salaam, wakati akizindua ripoti ya kujitathmini kwenye masuala ya utawala bora nchini (CRR), iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Kujitathimini kwa Nchi za Afrika (APRM).
Alisema kufuatia hatua zilizoanza kufanikiwa katika mapambano hayo, serikali itaendelea kuhakikisha yanaimarika zaidi, ili kuliwezesha taifa kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo.
“Kwetu ripoti hii ya APRM inatukumbusha falsafa na mtizamo wa Mwalimu Nyerere (Hayati Mwalimu Julius Nyerere), kupitia kitabu chake cha Tujisahihishe, alichokiandika mwaka 1962 na kile cha Mwongozo wa TANU alichokiandika mwaka 1971.
“Kujikosoa na kuchukua hatua katika muktadha sahihi kwa Waafrika, kutasaidia kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zetu ili kupiga hatua kwenye maendeleo ya kiuchumi. Hivyo APRM inachochea falsafa na mtizamo wa Mwalimu Nyerere,” alieleza.
Alisema baadhi ya changamoto zilizoibuliwa katika ripoti hiyo, zimeanza kufanyiwa kazi, ikiwemo suala la muundo wa serikali ya muungano, ambao umeelezwa kwenye katiba pendekezwa.
Samia alisema hadi sasa serikali imefanikiwa kutatua kero za muungano kutoka 97 hadi 25, ambazo nazo zipo kwenye hatua mbalimbali za kutatuliwa.
Changamoto nyingine iliyoibuliwa ni migogoro ya ardhi, ambapo Makamu wa Rais alieleza kuwa, serikali imechukua hatua katika kutatua migogoro hiyo, ikiwemo kutenga maeneo maalumu kwa wakulima na uwepo wa Mahakama ya Ardhi, ambayo inasaidia kuharakisha utatuzi wa migogoro hiyo kwa wakati.
“Lakini pia serikali imetunga sheria ya fidia na mipango miji, utoaji wa hati za umiliki ardhi, upimaji ardhi na uanzishwaji wa ofisi za ardhi kwenye kila kanda,”alisema.
Makamu wa Rais alizitaja changamoto zingine zilizoibuliwa kwenye ripoti hiyo ya kujitathimini kuwa ni tatizo la umeme na huduma za kijamii, ambapo tayari zimeanza kutauliwa kupitia mipango mbalimbali ya kiutekelezaji.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Azizi Mlima, alisema ripoti hiyo imehusisha maoni ya wananchi, wakielezea maeneo mbalimbali, ambayo serikali imefanya vizuri na yenye changamoto zinazopaswa kutatuliwa.
Alisema licha ya mpango huo wa kujitathimini kuhusisha nchi zote za Afrika, sio mataifa yote yaliyoanza kuutekeleza, hivyo Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizopiga hatua katika utekelezaji wake.
Mwenyekiti wa APRM- Tanzania, Profesa Hasa Mlawa, alisema awali, ripoti hiyo iliwasilishwa kwenye Baraza la Viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) nchini Ethiopia, mwaka 2013 na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.
Alisema baada ya kuwasirishwa kwa ripoti hiyo kwa muda wa saa moja, viongozi hao wa Afrika walipata wasaa wa kuijadali kwa zaidi ya saa nne, ambapo pamoja na changamoto mbalimbali zilizoibuliwa, Tanzania ilisifiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya demokrasia na utawala bora.
Profesa Mlawa alisema kumekuwepo na ushirikiano mzuri baina ya APRM na serikali, ambapo masuala muhimu yaliyoibuliwa kwenye ripoti hiyo, yamehusishwa katika utekelezaji wa mpango mkakati wa maendeleo wa taifa.
No comments:
Post a Comment