Monday, 18 September 2017
MAKONDA ATANGAZA NEEMA KWA WATUMISHI WA SERIKALI
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza neema kwa watumishi wa sekta ya elimu, afya, ulinzi na usalama, ambao sasa watauziwa viwanja kwa sh. 4,000, badala ya 15,000 kwa mita, katika maeneo tofauti ya mkoa huo.
Makonda alitangaza neema hiyo jana, alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, ambapo alisema mazingira ya kazi ya watumishi hao ni magumu na muda ni mdogo kutafuta kipato zaidi ili kumudu gharama kubwa za kununua ardhi.
Kutokana na hatua hiyo, alisema ipo haja ya kutafuta viwanja na kuwauzia watumishi hao kwa bei nafuu, ikiwemo kilichokuwa kikiuzwa mita moja kwa sh. 15,000, ambacho sasa watauziwa kwa sh. 4,000, ili waweze kumudu gharama za ujenzi.
“Kuna sababu nyingi zimenishawishi kugusa maisha ya mtumishi mmoja mmoja wa mkoa wangu. Watumishi hawa hawana muda zaidi wa kufanya biashara na kutafuta kipato cha kumudu kununua kiwanja kwa bei ghali,”alisema.
Makonda alisema watumishi hao wamekuwa wakinunua viwanja vya bei nafuu katika mazingira magumu, hivyo mkakati huo uliohusisha wadau wa ardhi, utawawezesha kununua viwanja sehemu yoyote wanayohitaji.
Mkuu huyo wa mkoa alisema, katika makubaliano na wadau hao wa viwanja, watumishi husika watapewa fursa ya kulipia kidogo kidogo kwa miaka mitano huku wakiendelea na ujenzi baada ya makubaliano kukamilika.
Pia, alisema amezielekeza manispaa zote za mkoa wa Dar es Salaam, kuhakikisha watumishi hao hawatozwi fedha katika hatua zinazoendelea za ujenzi.
“Katika kuhakikisha azma ya makazi bora inawafikia watumishi hao, nimeanza mazungumzo na wadau wa vifaa vya ujenzi ili wavipate kwa unafuu, kutokana na kipato cha maisha halisi ya askari, wahudumu wa afya na walimu,”alisema.
Alisema hadi sasa watumishi 37,000, wamejitokeza, wakihitaji huduma hiyo ya ardhi, ambapo kati yao, walimu ni 24,000, lengo likiwa ni kuwafanya kuwa na utulivu na kutohangaika na ugumu wa maisha hadi kufikia kushindwa huduma ipasavyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment