Monday, 18 September 2017
VIGOGO WALIOUZA PEMBEJEO FEKI MBARONI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inawashikilia vigogo wa kampuni kadhaa, wanaodaiwa kuhusika kuagiza na kuuza pembejeo feki za kilimo nchini.
Kukamatwa kwa vigogo hao, kumekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuiagiza taasisi hiyo kuwashughulikia wamiliki wa kampuni zinazodaiwa kuuza pembejeo feki kwa wakulima huku wakisababisha deni feki la sh. bilioni 48.
Msemaji wa TAKUKURU, Juma Misalaba, alisema Dar es Salaam, jana, kuwa vigogo hao walikamatwa hivi karibuni kwa nyakati tofauti na wameshaanza kuwahoji kuhusu tuhuma hizo.
Hata hivyo, Misalaba hakuwa tayari kutaja majina ya vigogo hao na idadi yao kwa madai kuwa, upelelezi bado unaendelea na endapo watafanya hivyo kwa sasa, wanaweza kuuharibu.
Alisema kazi hiyo inafanyika katika mikoa yote nchini na kwamba, wameamua kuifanya kwa umakini mkubwa kwa lengo la kupata vielelezo vyote muhimu vitakavyothibitisha madai hayo.
"Wakuu wetu wa TAKUKURU mikoani, wameshaanza kutekeleza agizo hilo la Rais Magufuli na tumeshawakamata wahusika kadhaa na kuanza kuwahoji kuhusu tuhuma hizo.
"Tukimaliza kuwahoji, wale wote watakaobainika kuhusika katika tuhuma hizo tutawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria na hilo linaweza kufanyika wakati wowote, lakini kwa sasa siwezi kutaja majina yao wala idadi,"alisema.
Misalaba alisema taasisi hiyo pia inazifanyia kazi tuhuma za wafanyakazi hewa 19,500, kaya masikini feki 56,000, zilizolipwa fedha na TASAF kinyume na taratibu pamoja na wanafunzi hewa 5,850, waliopata mikopo kwa ajili ya masomo ya vyuo vikuu.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alitembelea makao makuu ya TAKUKURU, mjini Dar es Salaam, ambapo aliwaagiza watendaji wake kutokuwa na kigugumizi cha kuwachukulia hatua watuhumiwa pale wanapopata ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma zinazowakabili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment