Monday, 18 September 2017

BOMU LAUA WATOTO WATATU


WATOTO watatu wa Kijiji cha Nafko, kilichoko kata ya Lokisale, wilayani Monduli, mkoani hapa, wamepoteza maisha baada ya kulipukiwa na bomu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema lilitokea juzi (Ijumaa), saa 2.00 asubuhi, wakati watoto hao wakichunga mifugo katika eneo la jeshi.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, watoto hao ni Dias Lengai (9), mwanafunzi wa darasa la pili, Sam Nyangusi (6), mwanafunzi wa darasa la kwanza na Lansis Saitabahu (8), mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi ya Kijiji cha Nafuko.

Alisema wakiwa machungani, watoto hao waliona kitu kama mpira, wakaanza kukichezea bila kujua kuwa ni bomu, ambalo kwa bahati mbaya lilipuka na wao kufariki papo hapo.

"Miili ya watoto hawa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na itazikwa leo kijijini Nafko,"alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Iddy Kimanta, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kuwataka wazazi kuongozana na watoto wao, hususan wanapochunga maeneo ya jeshi.

Alisema kwa bahati mbaya, watoto hao walikuwa peke yao wakichunga mifungo na walipoona bomu hilo (hakutaja aina yake), walianza kulichezea kama mpira na baada ya muda mfupi lililipuka na kuwasababishia vifo.

"Kambi ya Jeshi Monduli ina uhusiano mzuri na wananchi na mara nyingi  kipindi, ambacho siyo cha mazoezi ya kijeshi, wananchi wanaruhusiwa kuchunga mifugo katika eneo hilo. Vifo vya watoto hao vimetokea kwa bahati mbaya, naomba wananchi wawe watulivu,"alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema, wananchi wote wanaozunguka maeneo ya jeshi katika Wilaya ya Monduli, wana elimu ya kutosha juu ya kitu chochote ambacho siyo cha kawaida, watakachokiona wakiwa machungani au katika makazi yao.

"Jeshi kila wakati linatoa elimu kwa wananchi kuwataka kutoshika au kukisogelea kitu chochote wanachokiona wakiwa machungani kwenye maeneo ya jeshi, ambacho hawakifahamu na kukitolea taarifa kwa vyombo husika ili kiondolewe eneo hilo mara moja,"alisema

Kimanta alisema mara nyingi wananchi wakiwa machungani katika maeneo ya jeshi, wanapoona chuma chochote, hutoa taarifa ili kitu hicho kiondolewe, wananchi wasipate madhara.

Desemba, 2015, katika Kata ya Meserani, eneo la Lemomo, ambalo ni maalumu kwa mafunzo ya kijeshi, kijana aliyefahamika kwa jina la George Olodi (20), mkazi wa Lokisale, alipoteza maisha baada ya kukanyaga bomu na kumlipukia.

No comments:

Post a Comment