KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza serikali kwa kuweka kukamilisha kwa asilimia 98, ujenzi wa barabara ya Dodoma-Kondoa kwa kiwango cha lami, huku ikiwa imejengwa kwa kiwango cha juu.
Kutokana na ubora wa barabara hiyo, kamati imeiagiza serikali kuitunza ili iweze kutumika kwa muda mrefu kutokana na gharama kubwa zilizotumika katika ujenzi wake.
Aidha, kamati hiyo imeiagiza serikali kuhakikisha inajenga mzani kwa ajili ya kudhibiti magari yanayobeza mizigo mizito, ambayo yanaweza kusababisha iharibike baada ya muda mfupi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo, uliofanyika jana kwenye eneo la Mayamaya na Daraja la Kalema, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso, alisema wamefurahishwa na ujenzi wa barabara hiyo kutokana na kujengwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Alisema barabara hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa mikoa ya Dodoma, Manyara na Arusha kwa vile inaiunganisha kiusafiri na pia imehitimisha muunganiko wa barabara kutoka Afrika Kusini hadi Misri.
"Kwa kuwa ujenzi wa barabara hii umeigharimu serikali fedha nyingi, ni lazima itunzwe. Kuwe na mikakati ya kuilinda ili iweze kutumika kwa muda mrefu. Ulinzi na miundombinu na sheria za barabara vizingatiwe,"alisema.
Aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha inajenga mizani haraka iwezekanavyo ili kuzuia magari yenye uzito mkubwa kupita kwenye barabara hiyo na kuiharibu.
Pia aliagiza uharakishaji wa ulipaji fidia kwa watu ambao nyumba zao zilivunjwa kwa lengo la kupisha mradi huo. Alisema katika baadhi ya maeneo waliyopita, amesikia malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kucheleweshwa malipo yao ya fidia.
"Lazima ulipaji fidia ufanyike haraka. Ni kweli lengo la serikali ni kuwasaidia wananchi kiuchumi, lakini tutakuwa hatuuwatendei haki kama hatutawalipa fidia,"alisema.
Ili kuepuka ulipaji fidia usiokuwa na tija, Kakoso aliishauri serikali kuweka mapema alama za uhifadhi wa barabara, hasa katika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Joseph Nyamhanga, alisema ujenzi wa barabara hiyo umeigharimu serikali sh. bilioni 136 na umefanywa na kampuni kutoka China.
Alisema fedha za mradi huo zimetokana na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Shirika la Kimataifa la Misaada la Japan (JICA) huku serikali ikichangia asilimia mbili kwa ajili ya malipo ya fidia.
Nyamhanga alisema mradi huo umejengwa kwa awamu tatu na zote zimekamilika. Alisema asilimia mbili zilizobaki ni kwa ajili ya kumalizia kazi chache zilizobaki.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo umehusika Daraja la Kelema lenye urefu wa mita 205, ambalo limejengwa katika mto huo.
Katibu Mkuu alisema tayari wizara imeshafanya mazungumzo na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa ajili ya kujenga mzani ili kuepuka magari yanayozidi tani 56 kupita kwenye daraja hilo.
Aidha, alisema wakati wa ujenzi wa barabara hiyo, mkandarasi alijenga visima 14 kwa ajili ya matumizi ya vijiji mbalimbali na kwamba, vitakabidhiwa kwa vijiji hivyo kupitia kwa halmashauri husika.
Kwa mujibu wa Nyamhanga, barabara hiyo inatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali Oktoba 6, mwaka huu kwa mujibu wa mkataba na kuongeza kuwa, itakuwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja wa mkandarasi.
No comments:
Post a Comment