MWENYEKITI wa
Chama cha TLP, Augustine Mrema, amevunja ukimya na kuwaonya wafuasi wa CHADEMA,
wanaofanya dua maalumu ‘Albadir’ kwamba, wasitumie visivyo dini ya Kiislamu,
badala yake waviache vyombo vya dola vifanye kazi yake.
Kauli hiyo ya
Mrema inatokana na taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na Baraza la Vijana la
Chadema (BAVICHA), kutaka kusoma albadir,
kufuatia Mbunge wa chama hicho jimbo la Singida Mashariki,Tundu Lissu,
kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, nyumbani kwake mjini Dodoma.
Akizungumza
na gazeti hili jana, kwa simu, Mrema alisema watu wasitumie visivyo dini ya kiislamu
kufanya mambo ambayo hayapaswi kufanywa, kwa sababu vyombo vya dola vinaendelea
na kazi yake katika suala hilo ili watuhumiwa waliohusika waweze kukamatwa.
Mrema alisema
dini ya Kiislamu inaheshimika duniani, hivyo kitendo wanachofanya cha kusoma
dua, ni hatua kubwa mno kwani serikali haijaonyesha kushindwa kuwakamata
waliohusika na shambulio hilo.
Kwa mujibu wa
Mrema, wale wanaofanya kwa matakwa yao, ni vyema wakamatwe ili waseme ukweli.
Pia, Mrema
aliwataka Watanzania ambao wanazo taarifa kuhusu watuhumiwa hao, waiarifu
polisi ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Hivi
karibuni, Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alipiga
marufuku maandamano yaliyotangazwa na BAVICHA kwa ajili ya kufanya dua ya
albadir.
Licha ya
agizo hilo, BAVICHA walidai kuwa, wataendelea na mpango wao wa kumwombea dua
Lissu na kwamba, zuio la Mambosasa haliwahusu kwa sababu hawafanyi maandamano.
Juzi, Mwenyekiti
wa BAVICHA, Patrobas Paschal na Katibu Mkuu wake, Julius Mwita, walitimua mbio
na kuwaacha wafuasi wao watatu wakikamatwa na polisi, baada ya kutotii amri
iliyokataza kufanya dua hiyo.
Tukio hilo
lilitokea katika uwanja wa TIP, ulioko Sinza, jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia
suala hilo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema haoni
mantiki yoyote ya watu kusoma dua kwa sababu vyombo vya dola vinafanya kazi
yake.
“Unakimbilia kusoma
albadir ya nini, wakati vyombo husika vinafanya kazi, waliopigwa risasi ni
wengi, Sheikh wetu Ponda (Issa), alipigwa risasi hatujasikia watu wanafanya
kisomo.
“Watu wengi
wamepigwa risasi na wengine wamefanyiwa mambo yasiyofaa, hatujasikia watu
wanasoma albadir, Chacha Wangwe ameuawa huko hatujasikia albadir, Saanane (Ben)
amepotea mpaka leo hatujasikia watu kusoma albadir,” alisema.
Akieleza
maana ya albadir, Sheikh Salum, alisema ni kisomo au dua ambayo inatumiwa na viongozi
wa Kiislamu kwa mtu ambaye anataka kumshitakia
Mwenyezi Mungu, kutokana na dhuluma atakayokuwa amefanyiwa.
“Ukimshitakia Mwenyezi Mungu kwa jambo ambalo
ni sawa sawa, siyo kumshitakia kwa lile ambalo unataka kumuonea mtu.
“Au kumdhuru
mtu bila sababu, inatumika kwa watu ambao wamedhulumu wenzao, heshima yake au
chochote, basi unamshitakiwa kupitia dua
hiyo,”alisema.
Alisema
kwamba, albadir maana yake ni kuwataja maswahaba waliopigana vita vya Badir katika
mji wa Makha na sehemu hiyo imekuwa ikitumika kumshitakia Mungu.
No comments:
Post a Comment