JESHI la Polisi Tanzania, limeeleza kwamba
litaendelea kufuta leseni za madereva watakao bainika kutotii sheria za
barabarani bila ya kujali cheo au umaarufu wa mtu.
Pia, limeeleza kwamba kamwe haliwezi kumfumbia
macho dereva yeyote ambaye atabainika kufanya makosa ya kuhatarisha maisha ya
watu na mali zao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Kikosi
cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi Mwandamizi(SACP), Fortunatus
Musilimu, wakati akihojiwa na gazeti hili, ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Musilimu alisema
wanaendelea kufanya mageuzi katika kikosi cha usalama barabarani ili
kuzuia vifo kutokana na ajali na kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa.
Alisema amekuwa anafuatilia mienendo ya watendaji
wa kikosi hicho ili kujiridhisha na utendaji wao na wale wote wenye udhaifu,
atawaondoa kulingana na taratibu za polisi.
Kamishna huyo alisema mara alipotangazwa kushika
nafasi hiyo Julai 15, mwaka huu, kutoka kwa Kamanda Mohamed Mpinga, amekuwa
anafanya ziara za kushtukiza katika mikoa mbalimbali kwa lengo la kujitambulisha
na kujionea mwenyewe kazi jinsi zinavyofanyika .
Alisema tayari amefanya hivyo kwenye mkoa wa
Mbeya, ambapo alizifungia leseni za madereva saba wa magari baada ya kubaini wamekiuka sheria za nchi,
ikiwa ni pamoja na kusababisha ajali mbaya na vifo.
Pia, alifanya hivyo kwenye mkoa wa Arusha na
kufuta leseni za madereva 13, Manyara alifuta leseni za madereva wanne na
Kilimanjaro alifuta leseni 47 za madereva kutokana na makosa mbalimbali.
Kamanda Musilimu alisema leseni za madereva hao
zitafungiwa katika kipindi cha miezi sita, mpaka watakapojirekebisha utendaji
wao na kutii sheria bila shuruti.
Alitaja miongoni mwa sababu za kufuta leseni hizo
kuwa ni baadhi ya madereva kuwakuta
wakiwa wamelewa.
Akizungumzia kitendo cha polisi kutoza faini, alisema
jeshi hilo halikusanyi mapato na kusisitiza kazi
yao ni kuzuia uhalifu na kulinda mali za wananchi.
Kamishna
Musilimu alisema kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa askari
wamekuwa wanapangiwa kiasi cha kutoza faini kwa watu wanaobainika kufanya
makosa siyo za kweli.
Alisema serikali iliamua kutunga sheria ya watu
kulipa faini kupitia mihamala ya mitandao kwa lengo la kupunguza mrundikano wa
kesi.
Kamanda huyo alisema lengo la serikali ni kutaka
kupunguza mrundikano wa kesi katika mahakama hapa nchini, kitendo ambacho
kimepunguza kesi zilizokuwa zimefunguliwa kwa wingi katika mahakama mbalimbali.
Kamishna huyo alisema sheria itabakia kama
ilivyowekwa kwa makosa makubwa, ikiwemo kusababisha vifo au kuendesha gari
akiwa amelewa na kusababisha ajali.
Alisisitiza kwamba, kama watu wanafikiri serikali
inaendeshwa kwa mapato ya faini, wanafanya makosa.
Pia, alisisitiza kuwa hakuna askari yeyote wa
kitengo cha usalama barabarani aliyepangiwa kukusanya fedha kutokana na makosa
ya madereva.
Alisisitiza kuwa yeye na watendaji wenzake
watafanya kazi muda wote, iwe usiku wa manane au mchana, ndio maana amekuwa akiibuka
ghafla kufanya ukaguzi katika vituo mbalimbali na kuchukua hatua kwa askari
wote wanaofanya kazi zao kinyume na taratibu za jeshi hilo.
No comments:
Post a Comment