Tuesday 19 September 2017

MANJI KIZIMBANI SIKU TATU MFULULIZO





MFANYABIASHARA Yussuf Manji anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya, atatoa utetezi wake juu ya tuhuma hizo akiwa na mashahidi wake kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Septemba 25, mwaka huu.

Shauri hilo lililoko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, limepangwa kuendelea kwa ushahidi wa upande wa utetezi kwa siku hiyo, kutokana na kushindwa kusikilizwa jana.

Mfanyabiashara huyo alipanda kizimbani mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Mkeha, ambapo upande wa jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis huku yeye akiwakilishwa na Wakili Hajra Mungula.

Wakili Hajra alidai wapo tayari kuendelea na utetezi, lakini Wakili Vitalis aliieleza mahakama kuwa, anasafiri mchana na kwa kuwa shauri limechelewa kuanza, hawezi kuendelea.

Baada ya Wakili Vitalis kueleza hayo, Hakimu Mkeha alisema shauri hilo lilipangwa kuanza kusikilizwa saa tatu asubuhi, ambapo Manji aliomba msamaha na kueleza kuwa, alipitia hospitali na kabla ya hapo alikuwa akiwasiliana na wakili wake, ambaye alimweleza hakimu alikwenda kwenye kikao.

Hakimu Mkeha alisema alienda kwenye kikao Mahakama Kuu na alirudi mahakamani hapo mapema na anapaswa kwenda tena mchana.

Kutokana na hayo, Wakili Hajra aliomba shauri hilo kupangiwa siku tatu mfululizo kwa kuwa watakuwa wamemaliza ushahidi wao.

Hakimu Mkeha alitoa tahadhari kuwa tarehe itakayopangwa wafike mapema na shauri litaanza mapema na kuahirisha usikilizwaji wa shauri hilo hadi Septemba 25 hadi 27, mwaka huu.

Manji alitakiwa kutoa utetezi wake baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu, kutokana na upande wa jamhuri kujenga kesi yao.

Baada ya mshitakiwa huyo kuonekana ana kesi ya kujibu, shahidi wake wa kwanza, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi alishatoa ushahidi.

Mfanyabiashara huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Februari 16, mwaka huu, akidaiwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu,katika eneo la Upanga Sea View, Ilala, Dar es Salaam, alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

No comments:

Post a Comment