Tuesday, 19 September 2017
WATUHUMIWA SAKATA LA MISHAHARA HEWA WATIWA PINGU KIMYA KIMYA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), imepanua meno dhidi ya wahusika wa ubadhirifu kwenye fedha za TASAF, bodi ya mikopo na mishahara hewa, ambapo sasa wamedakwa na kuhojiwa kimya kimya.
Msako na mahojiano dhidi ya watuhumiwa hao, umekuwa ukiendeshwa kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha hakuna muhusika yeyote atakayekwepa mtego wa mamlaka hiyo.
Ubadhirifu kwenye taasisi hizo za serikali, uliwekwa bayana na Rais Dk. John Magufuli, wakati alipozungumza na watumishi wa TAKUKURU, Agosti 28, mwaka huu na kuwataka kuacha kigugumizi katika kuchukua hatua pindi wanapokuwa na ushahidi wa watu waliojihusisha na rushwa.
Rais Dk. Magufuli, alieleza namna anavyoshangazwa na mamlaka hiyo kutochukua hatua, licha ya serikali kubaini uwepo wa wafanyakazi hewa, kaya hewa masikini na wanafunzi hewa wasiopaswa kupewa mikopo ya elimu ya juu.
Aliitaka kuchukua hatua huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo katika vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Tangu Rais Magufuli alipotoa agizo hilo, TAKUKURU imekuwa ikiendesha uchunguzi dhidi ya wahusika, ambapo baadhi yao wamekwishafikishwa mahakamani huku watuhumiwa wengine wakihojiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji Mkuu wa taasisi hiyo, Mussa Misalaba, alisema uchunguzi na mahojiano yanafanyika kimya kimya ili kuhakikisha taarifa zote muhimu zinapatikana.
“Hii ni vita, hatuwezi kumweleza adui mbinu au aina ya silaha tunazotumia. Ngoma imefikia patamu, wahusika wote tunaendelea kuwahoji na hivi karibuni tutatoa taarifa kamili,” alieleza.
Alisema kutokana na sababu za kimkakati na unyeti wa mambo hayo, TAKUKURU imejidhatiti na kila muhusika atakayebainika, atafikishwa kwenye mamlaka husika.
“Hili ni zoezi endelevu na linafanyika nchi nzima. Uchunguzi umefikia kwenye hatua nzuri. Ninachowaomba Watanzania waendelee kutupa ushirikiano zaidi kwani tangu mwaka 2015, tumekuwa tukifanyakazi nzuri,” alieleza.
Hadi sasa, TAKUKURU imewakamata baadhi ya viongozi wa TASAF na kuwahoji huku ikiendelea kuchunguza jinsi pesa zinazodaiwa kulipwa kwa wahusika hewa, ikiwemo uthibitisho.
Misalaba alisema kazi hiyo inafanyika kila mkoa, ambako pesa za TASAF zilipelekwa na kulipwa kwa watu wasiostahili. Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya wahusika wote waliowahojia hadi sasa.
"Siwezi kukueleza majina yao, cha msingi agizo la Rais linafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na tumebaini baadhi ya mambo mazito, siwezi kusema kwa sasa, wakati ukifika tutasema,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment