Tuesday 19 September 2017

BULEMBO ABWAGA MANYANGA WAZAZI



MWENYEKITI wa Taifa wa Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alhaj Abdallah Bulembo, ametangaza kutowania tena nafasi yoyote ndani ya jumuia hiyo, kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.

Tayari Alhaj Bulembo alishachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, ambayo inaonekana kuwavutia wadau wengine kadhaa wa CCM.

Bulembo alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu kufanyika kwa uchaguzi wa wilaya, mkoa na ngazi ya taifa pamoja na dhamira yake ya kutogombea tena uongozi.

Alisema, Machi 9, mwaka huu, kulifanyika Baraza la Taifa la Wazazi, ambapo alitumia nafasi hiyo kuaga huku akisisitiza hatogombea nafasi yoyote ndani ya jumuia hiyo.

“Baadae nilisikia watu wakinitaka nigombee, nilichukua fomu. Pia, kuna wazee akiwemo Malecela (John) na Lusinde (Job), nao walifanya hivyo, niliamua kuchukua fomu. Tangu zamani dhamira yangu iliamua sitakuwa mgombea wa jumuia ya wazazi,”alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wanachama 49, wamejitokeza kuwania nafasi ya mwenyekiti, hivyo anaamini miongoni mwao kutakuwa na mtu mzuri atakayeiongoza jumuia hiyo.

Alisema jana, alitarajia kuwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ikieleza kuwa, hatogombea nafasi yeyote katika jumuia hiyo.

“Nilisema sitagombea, mara nyingi napenda kuongoza kipindi kimoja,”alisisitiza.

Akizungumzia mafanikio anayoyaacha katika jumuia hiyo, alisema tayari amejenga nyumba yenye ghorofa 14, iliyopo Mchikichini, viwanja 56 ambapo awali vilikuwa 16 na vyote vimepatiwa hati na alinunua pikipiki kwa ajili ya viongozi kwa lengo la kukiimarisha Chama na jumuia.

Pia, Bulembo alisema jumuia hiyo aliikuta ikiwa na deni la sh. bilioni 4.8, lakini waliweza kulipa kwa asilimia 65.

Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kuziboresha shule za jumuia hiyo, ambazo zilikuwa kama za watu binafsi na kwa sasa zinafanya vizuri kitaifa.

Mwenyekiti huyo alisema mapato nayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba, hadi sasa yamefikia sh. bilioni 1.4.

Hata hivyo, Bulembo hakutaka kuweka bayana kiasi cha fedha zilizopo hadi sasa katika jumuia hiyo, ambapo alisema wakati wa kukabidhi madaraka ataweka kila kitu hadharani.

Kwa mujibu wa Alhaj Bulembo, atakuwa tayari kutumwa na Chama kufanya kazi yoyote na kwamba, uongozi ndani ya CCM ni kupokezana kijiti, hivyo anamuacha mwingine aendeleze pale atapoishia.

Kuhusu uchaguzi ndani ya jumuia hiyo, Bulembo alisema wanayo matawi 23, 435 kati ya hayo, yaliyofanya uchaguzi ni 23, 431 na manne hayajafanya kutokana na migogoro ya wananchi na yapo katika mkoa wa Mbeya.

Bulembo alisema kata 3,958, kati ya 4,029, zimefanya uchaguzi, ambapo 71 uchaguzi wake ulifutwa kutokana na ukiukwaji wa kanuni na mbili zipo katika mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema uchaguzi ngazi ya majimbo 54 yaliko Zanzibra uchaguzi uliendelea vizuri na umefanikiwa kwa asilimia 100.

Hata hivyo, Bulembo alisema uchaguzi ngazi ya wilaya unatarajiwa kuanza kesho hadi Septemba 25, mwaka huu, nchini nzima.

Pia, alisema uchaguzi wa ngazi ya mikoa 32, unatarajiwa kuanza Novemba 7, mwaka huu hadi Novemba 9, mwaka huu, wakati ule wa taifa ni Novemba 20 hadi Novemba 23, mwaka huu, mjini Dodoma.

Alhaj Bulembo alisema viongozi watakaochaguliwa ni lazima wakiimarishe Chama na jumuia kwa kutafuta wanachama wapya na kuendeleza mema yaliyopo ndani ya CCM.

Alisema kipimo cha katibu wa jumuia hiyo wilaya ni kufanikisha uchaguzi na kwamba, atakayeshindwa kufanya hivyo, atakuwa amejiondoa mwenyewe katika nafasi yake.

Bulembo alisema kila mwenye kupata haki, aipate na kusiwepo na vitendo vya rushwa kwa wanaowania na aliwaonya wale wanaoanza kampeni za kuwaania nafasi mbalimbali kwamba waache

No comments:

Post a Comment